Tangazo

Pages

Friday, June 1, 2012

REAKING NEWS: BONDIA MAGOMA SHAABAN AFARIKI DUNIA




BINGWA wa zamani wa dunia wa ngumi za kulipwa uzito wa Super Fly, aliyekuwa akitambuliwa na WBU, Magoma Shaaban Ngereza amefariki dunia usiku huu katika hospitali ya Bombo, mkoani Tanga, imeelezwa.
Bondia maarufu wa zamani nchini, Ally Bakari ‘Championi’ amesema, Magoma aliyezaliwa Oktoba 21, mwaka 1980 mjini Tanga, amefariki majira ya saa 12 jioni.
Championi alisema kwamba Magoma alikuwa anaumwa kwa muda mrefu na siku nne zilizopita alizidiwa na kukimbizwa katika hospitali hiyo, kabla ya umauti kumfika leo.
Hadi anafariki dunia, Magoma (pichani kushoto) alikuwa amepigana jumla ya mapambano 16, akishinda 13, manane kati ya hayo kwa Knockout (KO), amepigwa matatu na yote kwa KO na hakuwahi kutoka sare.
Magoma alipanda ulingoni kwa mara ya mwisho Julai 21, mwaka 2006 na Eugen Sorin Tanasie mjini Timisoara, Romania katika pambano ambalo alipigwa kwa Technical Knocout (TKO) raundi ya pili.
Taji lake la kwanza kutwaa lilikuwa ni la IBF Afrika, Septemba 12, mwaka 1998 akimpiga Mkenya Joseph Waweru kwa KO raundi ya kwanza, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Mei 11, mwaka 2000 alimpiga bondia ‘matata sana’ Totin Lukunim wa Thailand na kutwaa taji la IBF Intercontinental, uzito wa Super Fly kwenye ukumbi wa PTA, Temeke, Dar es Salaam.
Agosti 3, mwaka 2001 ndipo alitwaa ubingwa wa dunia wa WBU baada ya kumpiga Ferid Ben Jeddou wa Tunisia kwa TKO raundi ya sita mjini Avezzano, Abruzzo, Italia, kabla ya kupoteza taji hilo kwa kupigwa na Gabula Vabaza Julai 26, mwaka 2002 katika ukumbi wa Hemingways Casino, East London, Eastern Cape, Afrika Kusini kwa KO raundi ya kwanza.
Mei 25, mwaka 2003 alipigwa na Mtanzania mwenzake, Mbwana Matumla kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam kwa TKO raundi ya nne.
Alijiunga rasmi na ngumi za kulipwa mwaka 1996, pambano lake la kwanza akicheza Juni 3, mwaka huo na kumpiga Athumani Omari kwa pointi, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Mungi aiweke pema peponi roho ya marehemu. Amin.

No comments:

Post a Comment