Tyson anavyofurahia maisha bila utajiri, umaarufu
*Alianzia maisha katika umaskini, akawa tajiri, amerudia umaskini
* Sasa hanywi pombe, hali nyama, anaishi maisha ya kawaida
MIKE Tyson kwa sasa anaonekana kuwa mzuri, pamoja na kuwa na tatoo usoni mwake.Anaonekana kuwa fiti, msafi na aliyetulia wakati akiingia Uingereza akiwa amevaa fulana iliyoandikwa “Team Tyson” .
“Ninaipenda England,” alisema huku akionekana kutabasamu huku akiwa ameunganisha mikono yake kama vile anasali. “Asante England,” alisema.
Mtu ambaye aliwahi kujiita mwenyewe kuwa ni mtu mbaya zaidi katika sayari sasa amebadilika na kuishi maisha ya aina yake.
Pia amekuwa si mlevi, hatumii dawa za kulevya na amebadili dini na kuwa mwislamu.
Amekuwa tofauti na kipindi ambacho alikuwa bado ulingoni ambapo aliwahi kutishia kuwala watoto wa wapinzani wake.
Mwandishi wa gazeti la The Sun la Uingereza ndivyo alivyoanza kuandika kuhusu Tyson ambaye amefanya ziara mwanzoni mwa wiki nchini Uingereza.
Aliendelea kusema aliwahi kukutana na Tyson mjini Las Vegas ambapo alikuwa akijiandaa kwa pambano lake dhidi ya Lennox Lewis.
Kipindi hicho mbabe huyo alikuwa akikenua na kuonesha meno yake yaliyokuwa na rangi ya dhahabu, alisema: "Ninazungumza na wanawake pale tu ninapotaka kufanya mapenzi nao.”
Kwa sasa, yuko tofauti, anaonekana kuwa mkarimu, kujichanganya na kuwa katika hali ya amani mwenyewe.
Bingwa huyo wa zamani wa ngumi uzito wa juu yuko London kwa ajili ya kuzindua nguo zake za ngumi( Mike Tyson Collection), ambazo zitakuwa zikipatikana London Fight Zone katika eneo la Lillywhites na kupitia sportsdirect.com.
Katika mahojiano na The Sun, Tyson mwenye umri wa miaka 46 alisema “Sijitambui jinsi nilivyokuwa.
“ Nilikuwa kama nimechanganyikiwa, lakini kitu hicho ndicho kilinifanya mimi kuwa mpiganaji mkubwa. Nilikuwa nikitaka watu wanakuja ulingoni kupambana na mimi kufikiri kuwa walikuwa wakishughulikana na mtu hatari mwangamizaji.
“Nilikuwa nikitaka wao kuonesha wananiheshimu. Nilikuwa kama nguruwe.Nguruwe."
Tyson amepambana ili kuweza kubadilika, vitu viwili vimesaidia katika maisha yake.
Kwanza ni kutokana na kifo cha binti yake aliyekuwa na umri wa miaka minne, Exodus kilichotokea Mei 2009, baada ya shingo yake kukabwa na mashine yake ya kufanyia mazoezi nyumbani kwa mama yake , ajali ambayo ilimsikitisha sana.
Siku 12 baada ya kifo hicho, Tyson alimwoa Lakiha “Kiki” Spicer (35), ambaye anamsifu kuwa amesaidia sana kubadili maisha yake.
Alisema: “Baada ya kifo cha Exodus nilijua kuwa nilihitajika kufanya kitu chanya na si kukaa pale na kuwa nimekasirika.
“Nilimwoa mwanamke wa ndoto zangu. Yeye ni mweusi kama mimi. Ninataka kufa naye.”
Tyson alikuwa akimjua Kiki tangu alipokuwa na umri wa miaka 13. Baba yake, Shamsud-din Ali, ni mwislamu ambaye ni kiongozi mkazi wa Philadelphia ambaye anahusiana na ulimwengu wa ngumi.
Kitu cha kwanza ambacho Kiki alimtaka kufanya ni kuacha kunywa pombe na kupunguza uzito.
Anasema: “Nilitakiwa kuchagua mlo wangu. Nilikuwa na uzito.Nilikuwa na umbo baya. Nikaja kuwa mlaji wa mboga.
“Niliacha kunywa pombe na kwa miezi sita nilikuwa nikila tomato tu na supu ya nyanya na maji.
“Nilipunguza uzito kilo 45 na sijala nyama kuanzia wakati huo. Sitaki kutumia kitu ambacho kitaninenepesha, situmii vyakula vilivyotayarishwa, wala nyama. Ni ngumu sana kuwa mtu mzuri kuliko kuwa bondia maarufu.
“Nilikuwa nikihitaji kuwa mtu mzuri na baba mzuri.”
Tyson kwa sasa anasema anataka kuwa baba mzuri wa watoto wake sita kwa kuwa hakuwahi kumjua baba yake wakati alipokuwa mdogo akikua.
Baba yake alitoweka na kumwacha yeye na dada zake ambapo walilelewa na mama yake ambaye alikuwa chapombe (mlevi) katika nyumba ndogo kwenye mji uliokuwa na halufu wa Brownsville, mji huo ulio nje ya New York hadi sasa umekuwa na matukio ya vurugu.
Tyson anasema awali alipokuwa shule alikuwa na sauti kali na alikuwa hajui kuongea vizuri. Alisema "Nilikuwa mnene na mwenye hasira. Watoto walikuwa wakinitania mimi.
“Kitu pekee kizuri ninachokumbuka kuhusu nilipokuwa mtoto ni njiwa wangu niliokuwa nikimfuga kwenye paa.”
Kisha , siku moja mtu mmoja alimchukua njiwa wake akamkata kichwa na kumnyunyizia damu mwilini mwake.
Tyson alimpiga mtu huyo. Alisema: “Nilijisikia vizuri. Kupiga ilikuwa ni kitu ambacho nilikiweza.”
Tyson aliendelea kuwa na tabia ya kupenda vurugu na alipofikisha umri wa miaka 12, alikuwa ameshakamatwa mara
38 na kuhukumiwa kifungo katika jela ya watoto ya Spofford Juvenile Center mjini Bronx.
Alisema: “Kwenda katika gereza la Juvenile ilikuwa kama ni kipindi cha kushangilia, kila mmoja alinijua jina langu .”
Muda mfupi baadaye alipokuwa kwenye shule ya kurekebisha tabia ndipo alipoonwa na bondia wa zamani Bobby Stewart na kutambua kipaji chake na kumwahidi kumsaidia kama atajituma katika masomo yake.
Wakati Tyson alipokuwa na miaka 13, Stewart alimchukua na kumpeleka kwa kocha wa ndondi Cus D’Amato ambaye alianza kumnoa.
Pia alikuja kuwa mwangalizi wake kisheria wakati mama yake Tyson alipofariki miaka mitatu baadaye. D’Amato ndiye alimbadili Tyson hadi kuja kupata mafanikio makubwa zaidi, akawa tishio kwa mabondia wa rika lake.
Mwaka 1986 aliweka historia ya kuwa bondia wa kwanza mwenye umri mdogo zaidi kutwaa ubingwa wa ngumi wa uzito wa juu akiwa na miaka 20, lakini mshauri wake mkuu D’Amato alifariki mwaka mmoja kabla.
Bundi huyo akaja kutawala ngumi.
1992 alikutwa na hatia ya kumbaka mrembo Desiree Washington na akaja kuhukumiwa kifungo cha miaka sita jela. Akiwa jela alibadili dini nakuwa mwislamu. Baada ya kuachiwa, alikutwa na janga la kujiharibu mwenyewe kwa mara nyingine.
Anasema: “Nilikuwa nikinywa chupa za pombe za dola 3000 kwa siku na kutumia cocaine usiku mzima, kisha kulala na ninapoamka kuendelea kunywa tena.”
Hadi kufikia mwaka 2003, alikuwa ametumia fedha zake na kupoteza utajiri wake wenye thamani ya dola milioni 300 na akaja kutangazwa kuwa amefirisika.
Anasema: “ Haikuwa jambo la kujali. Sikuweza kuzimiliki fedha. Kwangu pesa ilikuwa na maana (kuzitumia) pombe na madawa.”
Desemba 2006 Tyson alikamatwa kwa kukutwa na dawa za kulevya na kuendesha gari akiwa amelewa madawa. Baadaye aliwekwa gerezani na kutozwa faini.
2007 aliamua kwenda kwenye kituo cha ushauri nasaha cha Wonderland Center, kilichopo Los Angeles ambako alipata tiba ya ushauri.
Anasema: “Nilitoka, nikakutana na Kiki na maisha yakaja kua mazuri.”
Kwa sasa, Tyson amekuwa akifanya kazi za majukwaani na kwenye runinga. Aliigiza katika filamu ya Hangover (ambayo inamwelezea mwenyewe) na katika Broadway katika shoo ya Undisputed Truth.
Anasema: “Ninataka kuwaburudisha watu. Ninataka tuzo ya Tony . Wakati mwingine huona kama sistahili kuwa pale
. Hufikiria kuwa ningekuwa nimekufa. Niko katika umri wa miaka ya 40. Sikutarajia kufikisha miaka 25."
“Nilikuwa mtu mbaya, nilikaba watu. Nilipiga risasi. Nimefanya mambo mengi ambayo siwezi kujivunia.”
Sasa, anaelekeza macho yake kwa mwingereza Ricky Hatton,bingwa wa zamani wa ngumi duniani uzani wa welter , ambaye anarejea ulingoni baada ya kustaafu miaka mitatu iliyopita.
Tyson anasema ni kitu kizuri kwake kurejea katika ngumi na kama atapigana kama alivyokuwa mwanzo fujo na hasira atafurahia.
Tysona anasema hawezi kurejea tena katika ngumi baada ya kustaafu.
“Unaweza kunipatia ofa ya dola bilioni moja na nitasema 'Hapana'. Kwa sasa nina amani. Niko katika sehemu ambayo nilitakiwa kuwa katika maisha.”
Jina kamili : Michael Gerard (Malik Abdul Aziz)
Jina bandia: Iron Mike
Alizaliwa: Juni 30, 1966
Umri miaka 46
Urefu: futi 5. inchi 10
Rekodi yake: Kushinda mapambano 50 (44 kwa ko), kupigwa sita, mawili kufutwa matokeo
Alitwaa ubingwa wa: WBC, WBA na IBF, ikiwemo kushikilia mikanda yote
Alipata fedha kiasi cha dola 300 (pauni mil. 188)
Alifungwa miaka sita (akatumikia mitatu) kwa kumbaka, Desiree Washington
Ameoa mara tatu, Mwigizaji Robin Givens, 1988-89; Daktari Monica Turner, 1997-2003; Binti wa kiongozi wa dini, Kiki Spicer kuanzia mwaka 2009.
Ana watoto sita
Pambano linalokumbukwa: Ni la mara ya pili dhidi ya Evander Holyfield mwaka 1997. Tyson alisimamishwa ngumi kwa kumng'ata na kumnyofoa sikio mpinzani wake.
Makala haya yametafrisiwa na mwandishi Deodatus Myonga kutoka gazeti la The Sun la Oktoba 10,2012.
Duh ninomaaa jamaa alikuwa hatari sana
ReplyDeleteHatarii ilo balaa la njiwa kaka
ReplyDelete