Na Onesmo Ngowi
Masumbiwi
au kwa majina mwengine ndondi au ngumi na kwa majina ya mitaani ndogwa,
mawe n.k. ni mchezo unapoendwa sana na watu wengi. Aidha mchezo huu ni
kati ya michezo inayoogopwa sana duniani. Mchezo wa ngumi uko hatarini
kupoteza maana yake ya asili yaani kucheza kama burudani, kuwakilisha
nchi na kujenga ushupavu wa mchezaji. Mamilioni ya watu wanaojazana
kuutazama wasingependa kabisa kujiingiza kuucheza mchezo wa ngumi. Sasa
endelea………………………………….!
Kuna
ngazi mbalimbali katika mchezo ngumi zinazompa mdau yeyote nafasi ya
kushiriki katika kuuendeleza mchezo wenyewe kwa jinsi anavyotaka. Ngazi hizi
zimetejwa wazi wazi na sio lazima mtu awe tu kiongozi ndipo aweze
kuchangia maendeleo kwenye mchezo wa ngumi. Baadhi ya ngazi zilizotajwa
ni urefarii, ujaji, utunza muda, mtamngazaji wa ulingo, mkuzaji,
mdhamini, meneja, kocha, mpanga mabondia nk. Mdau yeyote anayetaka
kuchangia maendeleo ya mchezo wa ngumi anaweza kuchukua moja ya nafasi
kati ya zilizotajwa hapo juu.
Hakuwezi
kuwa na maendeleo kwenye mchezo wa ngumi kama wahusika waliotajwa hapo
juu hawapo. Ni lazima kuwe kwanza na bondia na timu yake ya meeneja,
kocha n.k ndipo promoter aweze kuandaa mpambano na mpinzani aliye na
safu ya watu kama hao. Katika nchi zilizoendelea hususan Marekani na
nchi nyingi za Ulaya bondia anatakiwa awe na kiwango kizuri ili ajiunge
na ngumi za kulipwa. Kwa kuwa mchezo wenyewe wapenzi hulipa fedha nyingi
kuuagalia wanategemea kuona mchezo mzuri hivyo wahusika lazima wawe na
viwango vizuri vya ngumi.
Katika
miaka ya 50 hadi 60 mabondia wengi wa ngumi za ridhaa waliokuwa
wanashiriki na kushinda medali kwenye michezo ya Olympic, Jumuiya ya
Madola, michezo ya majeshi ya dunia na mashindano mengine ya kimataifa
walikuwa wakipata mameneja na mapromota wazuri kuanza michezo ya ngumi
za kulipwa.
Mfano
mzuri ni bondia Robert Wangila Napungi wa Kenya aliyeshinda medali ya
dhahabu kwenye mashindano ya Olympic yailiyofanyika Korea ya Kusini
mwaka 1988. Aliporudi tu nyumbani kwake Kenya mameneja wengi maarufu wa mchezo huo duniani walipigania kumchukua kwenye Kampuni zao.
Madau
mbalimbali ya fedha yalitolewa na mameneja/mapromota hao hatimaye Bob
Arum mmoja wa mapromota wakubwa duniani mwenye makao yake jijini Las
Vegas, Nevada, Marekani akashinda na kumchukua. Kwa kuanzia tu Bob Arum
alitoa kitita kisichopungua dola za Kimarekani laki 2 na nusu ili kupata
sahihi ya Wangila ambaye alikuwa hajui hata baba yake mzazi (kwani
alituzwa na nyanya yake tu). Kwa muda mfupi tu aliweza kununua nyumba
ghali na ya kifahari kwenye eneo la Muthaiga ambalo hujulikana kuwa ni
la matajiri jijini Nairobi pamoja na magari ya kifahari kabla hata
hajarusha ngumi moja ya kulipwa.
Viwango
vizuri vya bondia anayeanza ngumi za kulipwa ndivyo vinavyoweza
kumhakikishia bondia mwanzo mzuri kwenye ngumi za kulipwa. Lakini
viwango hivyo sio kikwazo kwa bondia kujiunga na ngumi za kulipwa. Wapo
mabondia wengi wa miaka ya karibuni waliong’ara kwenye medani ya
kimataifa bila ya kushiriki au kuwa mabingwa wa mashindano ya Olympic au
Jumuiya ya madola. Kundi hili linaongozwa na bondia anayejulikana sana kwa wengi kama kielelezo cha mchezo huu kwa miaka ya karibuni, bondia Mike Tyson wa Marekani.
Bondia huyu sio tu kama alikuwa bondia wa kwanza wa umri mdogo kuwahi kuwa bingwa wa ndondi wa uzito wa juu duniani, bali alikuwa pia bondia wa
kwanza kuweza kupata kitita kikubwa cha fedha toka kwenye ngumi. Wakati
Tyson alipokuwa bingwa wa uzito wa juu duniani alikuwa na umri wa miaka
20 na aliweza kukusanya zaidi ya dola za Kimarekani milioni 300 kiasi
ambacho hakijawahi kufikiwa na bondia mwingine yeyote duniani. Pamoja na
kwamba fedha nyingi kati ya hizo zilitumika vibaya kwa ajili ya ushauri
mbovu ni dhahiri kuwa kwa fedha hizi Mike Tyson alikuwa mmoja wa
matajiri waliotukuka duniani.
Kwa
hapa Afrika tunao mabondia walioweza kujikusanyia fedha na sifa nyingi
katika medani ya mchezo huu wa ngumi. Baadhi yao wakiongozwa na Dick
Tiger wa Nigeria, John Kotey wa Ghana, Azumah Nelson wa Ghana, Lottie
Mwale wa Zambia, Ayubu Kalule, Bonza Edward na John Mugabi wote wa
Uganda pamoja na utitiri wa mabondia wa Africa ya Kusini wakiongozwa na
Dingan Thobela (Rose of Soweto) Baby Jacky Matlala, Francis Botha na
wengine wengi. Nchini Tanzania tumebahatika kuwa na baadhi ya mabondia
mabingwa wa Dunia wa vyama vya ngumi kama WBU, IBU, UBO mabondia hawa ni
Rashid Matumla, Magoma Shaban, Mbwana Matumla, Francis Cheka na Karama
Nyilawila.
Kama
nilivyokwisha eleza hapo juu viwango na misingi mizuri ndiyo njia pekee
ya mafanikio mazuri kwenye ngumi. Wengi wa mabingwa wa ngumi toka
Afrika wanapata
nafasi ya kuwa mabingwa wa dunia kwa kuongozwa na mameneja au mapromota
toka nje ya bara hili. Hii imetokana na uelewa pamoja na uwezo wa
kifedha wa mameneja na mapromota hao toka nje ya Afrika.
Ili
kumpata bondia mzuri atakayeweza kushinda vizuri meneja au promota wa
bondia hana budi kuwekeza kwa bondia husika. Kwa maana nyingine bondia
ni kama mtambo wa meneja au promota wa kuzalisha fedha. Ili mtambo
wenyewe uweze kuzalisha fedha hauna budi kuandaliwa na kutunzwa vizuri.
Hatua mbalimbali zinatakiwa zifuatwe ili bondia aweze kuwa mwenye nafasi nzuri ya kutengeneza fedha.
Hatua hizi ni kama ifuatavyo; Meneja anapaswa kumtafutia bondia wake kocha aliye na uwezo wa kumwandaa
ili awe na hali mzuri kimchezo wakati wowote. Meneja anatakiwa awajue
wapanga mabondia (Matchmakers) mbalimbali ambao hutumiwa na mapromota
kuwapanga mabondia katika mapambano wanayoandaa. Meneja anatakiwa ampate
daktari atakaye mhudumia bondia wake wakati wowote ule.
Meneja
anatakiwa kuhakikisha kuwa anavyo vifaa muhimu vya kumwandaa bondia
wake pamoja na lishe bora. Meneja anatakiwa kumtetea bondia wake katika
mikataba mbalimbali ili wote wanufaike. Meneja anatakiwa amlinde bondia
wake asipigane mara nyingi kuliko anavyotakiwa ili kuzuia asije akachuja
kimchezo. Yote haya yanahitaji fedha kwa hiyo meneja anatakiwa awekeze kwa bondia muda mrefu ili fedha zake ziweze kurudi na hatimaye atengeneza faida.
Mabondia
wengi hapa Afrika hususan Tanzania hawana mameneja wenye uwezo wa kuwa
meneji. Ama watu wenyewe wanaojiita mameneja hawajui maana halisi ya
kumeneji mabondia au ni watu wanaotaka tu kumtumia bondia kwa manufaa yao wenyewe. Mabondia nao hawajui taratibu husika za kuwa na meneja mzuri.
Wenzetu
wa Ulaya na Marekani hata Asia na Amerika ya Kusini na baadhi ya nchi
za Africa wamepiga hatua kubwa kwenye jambo hili. Hii inatokana na
ukweli kwamba mchezo wa ngumi unahesabika kama ajira na kuheshimiwa na serikali za nchi zao.
Bondia
wa kulipwa na baadhi ya mabondia wa ngumi za ridhaa wanalipa kodi
kutokana na mapato anayopata. Hali hii inawaweka katika nafasi nzuri ya
kuwa na mtiririko mzima wa uongozi katika mchezo wenyewe. Serikali za
wenzetu zinathamini michango inayotolewa na michezo ya ngumi sio tu kwa
kuwaletea mikanda ya ubingwa bali kwa kuchangia kwenye pato la taifa.
Pambano moja tu ambalo bondia Mike Tyson alilocheza na Lenox Lewis
liliingiza zaidi ya dola za kimarekani milioni 780.
Fedha
hizi zinatokana na ulipaji wa matangazo mengi ya kibiashara wakati wa
matayarisho ya mpambano na siku yenyewe ya mpambano. Kituo kimoja tu cha
television kinaweza kumlipa promota wa mpambano kiasi cha mamilioni ya
dola za kimarekani ili kurusha pambano lenyewe. Kituo hiki baadaye
kinaviuzia mpambano huu vituo vingine vya television vya nchi mbalimbali
na hivyo kutengeneza fedha lukuki. Hii ndio sababu bondia mmoja anaweza
kulipwa kiasi cha dola za kimarekani milioni 20 na kuendelea.
Utaratibu
huo wa kupromoti na kutangaza biashara hapa kwetu Afrika hususan
Tanzania bado haujaanza kueleweka. Ni nchi chache sana Afrika ambapo
vituo vya television vinaweza kulipa promota wa pambano fedha ili
walirushe kwa watazamaji wake. Nchini Afrika ya Kusini na Namibia kuna
utaribu wa television kuwalipa mapromota angalau fedha kiasi kwa ajili
ya kurusha mapambano ya ngumi. Utaratibu huo hapa kwetu Tanzania bado
haujaanza.
Kiasi
cha fedha nyingi ambazo bondia hulipwa hutokana na fedha zinazotoka
kwenye matangazo ya biashara. Nyingi ya fedha hizi zinaweza tu
kupatikana kama vituo vya television vinarusha mapambano husika. Namna
nyingine ya kupata fedha kwenye promosheni ya mpambano wa ngumi ni kwa
kampuni mbalimbali zinazotaka kutangaza bidhaa zao. Kampuni hizi ama
hutumia mpambano husika au bondia mmoja mmoja kwa kuingia naye mkataba
wa kuitangazia biashara zake. Japokuwa utaratibu huu umeshaanza kutumika
hapa Tanzania lakini kiwango chake ni kidogo sana.
Maajenti
mbalimbali wa matangazo ya biashara ndio husimama kati ya kampuni hizi
na wanamichezo. Sio rahisi bondia kujipeleka mwenyewe kwenye kampuni
husika kwa minajili ya kutafuta mikataba. Mameneja wa mabondia wanatakiwa
wawatafutie mikataba mbalimbali yenye manufaa kwa wote wawili.
Makampuni nayo yanatakiwa yaelewe dhana nzima ya kuwatumia mabondia
kupromoti bidhaa zao. Juhudi hizi za kuelimishana zinatakiwa zifanywe na
taasisi za michezo zikishirikiana na vyombo husika vya dola.
Kwa
kuwa michezo hususani ngumi ni ajira inatakiwa ipewe kipaumbele na
serikali ili iweze kuchangia pato la taifa. Serikali ikiweza
kushirikiana vyema na vyama au taasisi husika mchango wa mchezo wenyewe
unaweza kuchangia kupunguza tatizo la ajira.
Ikumbukwe
kwamba bondia mmoja tu anaweza kuwapa watu wafuatao kazi: Meneja,
Kocha, Daktari, Cutman, Mechi Meka, Promota, Refarii, Jaji pamoja na
watu wengi wanaouza bidhaa na huduma kadhaa wa kadha. Tukiwa na mabondia
wengi walio kwenye viwango vizuri ni wazi kwamba namba ya watu
waliotajwa hapo juu ingeongezeka kwa kiasi kikubwa. Mchango wao katika
pato la taifa ni mkubwa sana kwani kila mmoja wao atalipa kodi na
kutunza vyema familia yake. Iaendelea………………………….!
No comments:
Post a Comment