Tangazo

Pages

Monday, October 29, 2012

MCHEZO WA MASUMBWI, TAA INAYOZIZIMA – SEHEMU YA KUMI NA TISA

UNAPENDWA NA KUOGOPWA NA WATU WENGI DUNIANI
■UKO HATARINI KUPOTEZA ASILI YAKE KABISA


Na Onesmo Ngowi


Masumbwi au kwa majina mwengine ndondi au ngumi na kwa majina ya mitaani ndogwa, mawe n.k. ni mchezo unapoendwa sana na watu wengi. Aidha mchezo huu ni kati ya michezo inayoogopwa sana duniani. Mchezo wa ngumi uko hatarini kupoteza maana yake ya asili yaani kucheza kama burudani, kuwakilisha nchi na kujenga ushupavu wa mchezaji. Mamilioni ya watu wanaojazana kuutazama wasingependa kabisa kujiingiza kuucheza mchezo wa ngumi. Sasa endelea………………………………….!


Ari ya kucheza gumi ya Duran na kiu chake cha kupata fedha nyingi zilimfanya apande uzito kwenda Welter. Miaka ya sabini ilimshuhudia Roberto akipata ushindi wa uhakika kwa kuwanyuka vilivyo mabondia kama Carlos Palomino ambaye alikuwa bingwa wa zamani wa dunia wa welterweight aliyetambuliwa na WBC) na Zeferino“Speedy” Gonzales. Ikumbukwe kwamba mabondia hawa wawili walikuwa kati ya kundi lililokuwa tishio kwenye uzito wa Welter!


Kuingia kwa Duran kwenye uzito huu hasa ikikumbukwa kuwa alikuwa anamfuata mbabe mwenzake Sugar Ray Leonard ambaye tayari alishajijengea sifa kibao kwenye daraja hilo kulitafsiriwa kuwa ni kiama kwa mabondia wengine. Wachezeshaji kamati wengi (Betting Houses) walingojea kwa hamu habari za kutangazwa kwa mpambano utakaowakutanisha miamba hiyo miwili!


Ilifiki siku ya siku ambayo kila mpenzi wa masumbwi duniani alikuwa anaingojea kwa hamu. Tarehe na mahali pa mpambano wa mwaka ilipangwa nayo ilikuwa si pengine ila Uwanja wa Olimpiki jijini Montreal mahali ambapo Sugar Ray Leonard alijipatia medali ya dhababu ya Olimpiki mwaka 1976.


Mpambano huu kama walivyoelezea wanazuoni wa maaswala ya ngumi uliwakutanisha mbabe wa ngumi wa miaka ya sabini na bingwa wa miaka ya baadaye, miaka ya themanini pamoja nao alikuwepo pia bondia machachari toka Mexico Julio Cesar Chavez.


Sugar Ray Leonard ambaye ndiye aliyekuwa bingawa wa dunia wakati huo baada ya kumshushia kipigo kisichokuwa na wasiwasi mbabe toka Puerto Rico, Wilfred Benitez. Hakika Ray Leonard alikuwa ndiye kipenzi cha vyombo vingi ya habari na hakuna aliyeamini kama mbabe huyu angepoteza ubingwa wake kwa “mikono ya mawe” (Hands of Stone) toka Panama City!

Kupendwa kwake Ray Leonard na vyombo vya habari pamoja na wachezesha kamari (Betting Houses) zilimpa shinda Duran na alijiona kama anapamana na mataifa yote ya American ya Kaskazini ambayo ni Marekani na Kanada.


Mgao wa fedha za mpambano nazo zliichemsha harisa ya Duran na akajiona kwamba kumbe kweli kulikuwa hamna haki kwake. Ray Leonard alikuwa ndiye achukue zaidi ya robo tatu ya kitita cha mpambano ukilinganisha na cha Duran ambacho kilikuwa ni robo tu. Haya yote yalimchukiza sana Duran na aliapa kwamba angemuulia Ray Leonard ulingoni!


Hasira za Duran kwa Ray Leonard hazikuwa ndogo, kwani wakati wa mkutano wao na waandishi wa habari alimtukana na kumkebehi kama kweli alikuwa mwanamme. Alienda mbali hata kumtukana mkewe Juanita!


Haya yote yaliongeza msisimko wa mpambano na mashabki wengi wa ngumi walingojea kuuona moto utakaowashwa kwa mikono ya miamba hiyo miwili! Lengo la Duran kumshambuliwa Ray Leonard lilikuwa kumtibulia ili asiweze kufikiria vyema na baadaye kumtoa nishai ulingoni.


Mshikemshike wa Montreal “Brawl in Montreal” wa tarehe 20th, Juni 1980 ndivyo mpambano huu ulivyopewa jina na vyombo vingi vya habari na ulingojewa na kila mtu anayependa ngumi.


Ilikuwa ni siku ya mvua nzito na japokuwa kulikuwa na baridi kwani kipindi cha baridi ndio kilikuwa kinaishia maelfu kwa maelfu ya wapenzi wa ngumi waliohudhuria bila manunguniko kwani walijikuta wakisisimka kutokana na mpambano huo mkali wa aina yake.


Kama kawaida yake Ray Leonard ambaye kwa maumbile ndiye aliyekuwa mkubwa alianza kwa kuutumia vilivyo ukumbwa wa ulingo kwa staili yake ya kurukaruka na kuchezacheza. Mashabiki waliufuatilia mwendo wake wa madaha kwa kelele za muue, muue huyo Mpanama Ray!


Naye Duran alikuwa anamfuata Ray Leonard kwa usongo wa kummaliza kama mtu aliyepagawa na akitaka kuugeuza mpambano wenyewe uwe vita ya msituni.


Hakika hii ndiyo iliyokuwa staili Duran aliyoizoea kwani mapambano yake mengi yalikuwa hayana tofauti na mapigano ya kwenye vita vya msituni. Kwake mpambano wowote ulikuwa ni vita kwelikweli!


Usongo wa kurusha makonde kwa kinyongo na ushambuliaji mkali wa Duran uliweza kumpatia raundi ya kwanza bila shida. Hii ilimpa nafasi ya kujipongeza na kujipa moyo kwamba kumbe kelele za Ray Leonard hazikuwa kitu chochote. Lakini kwa maelfu ya mashabiki waliojazana kwenye ukumbi huo wa Olimpiki mjini Montreal kwao raundi hiyo ilikuwa ni kama asusa tu ya mpambano huo wa mwaka!


Kwa usemi usemeo kwamba “siku njema huonekana asubuhi” ilidhihirisha na ushindi wa raundi ya mwanzo uliompa joto Duran akaingia raundi ya pili kama mnyama aliyetaka kukitafuna kitoweo chake sawasawa. Kwa uhakika raundi ya pili ilikuwa ni kipigo kikali kwa Ray Leonard kwani mwishioni mwa raundi Duran alimpambikizia Ray Leonard konde zito linaloiwa “right-left combo” likifuatliwa na ngumi aina ya hook ya mkono wa kushoto iliyoingia barabara usoni mwa Ray Leonard.


Uzito wa konde hilo la Duran kwenye uso wa Leonard ulileta wasiwasi kwenye kona yake na japokuwa Ray Leonard alitingisha kichwa na kuchezacheza lakini ukweli ni kwamba kila mtu alijua kuwa amepewa kibano cha uhakika. Watu wengi hususan mashabiki wa ngumi waliojazana kwenye ukumbi huo walianza kushuku kama kweli Ray Lenaord angeweza kumaliza mpambano huo!


Baada ya kupewa kibano kwenye raundi hiyo Ray Leonard aliamua kutumia sehemu ya ndani ya ulingo ambayo asingeweza kuangushwa kirahisi na makonde ya mbabe wa Panama City kwa kweli hiyo ilimpa nafasi ya kuuonyesha ulimwengu uwezo aliokuwa nao kwenye ngumi!


Baada ya raundi kumi na nne za kuadhibiana vikali watu wengi walioona wazi kuwa Duran angeshinda mpambano huo na kwa kweli hata yeye mwenyewe aliona uwezekano huo! Mikono ya mbabe huyo toka Panama City yalirindima kwa ushuhuda wa kusukuma makonde ya mfululizo yaliyokuwa yanaingia barabara kwenye uso wa Ray Leonard. Ilikuwa ni muda tu ulimwengu utambue kweli nami mbabe kati yao!


Mwanzoni mwa raundi ya kumi na tano na ya mwisho Duran alikataa kugusana glovu na Ray. Ni kawaida ya mabondai wanapofikia kucheza raundi ya mwisho kugusanisha glovu kuonyesha kuwa wao ni wanamichezo na sio maadui. Lakini kwa Roberto Carlos Duran hii kwake ilikuwa ni vita na mtu aliyesimama mbele yake Sugar Ray Leonard alikuwa adui namba moja! Alilazimishwa na refarii wa mpambano huo Carlos Padilla kugusanisha glovu!


Raundi hii ilimshuhudia Duran akimkebehi Ray Leonard kwa makonde ya mpapatiko (telling punches) na ulizi uliomnyina nafasi kabisa ya kufikisha ngumi zake kwa Duran. Ikumbukwe kwamba kwa sababu ya tofauti ya lugha Duran alishikwa sana na hasira kuwaona mashabiki wengi wakipiga kelele.


Duran alikuwa anazungumza kugha ya Kihispania wakati sehemu yenyewe Montreal alikopigania kunazungumzwa lugha za Kiingereza na Kifaransa. Kelele za mashabiki zilimzidishia hasira Duran kwani hakuelewa kama walikuwa wanamtukana au kumshangilia.
Inaendlea…..!


Mwandishi wa makala haya ni; Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC), Shirkisho la Ngumi za Kulipwa Afrika Mashariki na Kati (ECAPBF), Shirikisho la Ngumi la Kimataifa bara la Afrika, Masharilki ya Kati, Ghuba ya Uarabu na Uajemi (IBF/AFRICA) na Mkurugenzi wa Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola (CBC) E-mail: ibfafrica@yahoo.com

No comments:

Post a Comment