Tangazo

Pages

Tuesday, April 16, 2013

GHANA KUTAWAKA MOTO MEI 3, MAPAMBANO MATATU YA IBF YAJA


FOR IMMEDIATE RELEASE – MONDAY 15, 2013 - Dar Es Salaam - Nchi ya Ghana ambayo ni moja ya nchi zenye vipaji vingi vya wanamichezo mahiri na majina makubwa hususan mchezo wa ngumi, itawaka moto tarehe 3, Mei wakati mabondia mahiri sita watakapogombania mataji ya IBF katika ubingwa mbalimbali.

Bondia atakayeanza kupanda ulingoni kufukisha moto huo ni “Mtoto wa Kijiweni” Albert Mensah ambaye amejizolea sifa kemkem za kupambana na mabondia mahiri duniani. Mensah yuko kwenye viwango vya IBF vya dunia na amewekwa namba 7 kwa ubora duniani katika uzito wa Welter.
 
                 Helen Joseph
Mbabe huyu atakumbana na bondia mwenye maringo na “Mtoto wa Mjini” Ben Odamettey ambaye amekulia katika viunga vya Jamestown katika kata ya Bukom jijini Accra, ambayo ni maarufu kwa kutoa mabingwa wengi wa dunia kama kina Azumah Nelson, Ike Quartey, Joseph Agbeko na Poison Kotey. Wawili hawa watapambana kugombania ubingwa wa IBF katika bara la Afrika uzito wa Junior Middleweight.
               Marriana Gulyas (kushoto)
 
Mpambano wa pili na unaongojewa kwa hamu kubwa ni ule wa mwanadada na mrembo kutoka Nigeria ambaye anaishi nchini Ghaba, Helen Joseph atakapombana na binti Mfalme kutoka Himaya ya Austrohungrian (Hungary) bi. Marianna Gulyas. Warembo hawa wanagombania mkanda wa IBF wa Mabara wa wanawake katika uzito wa unyoya (Featherweight) na moto mkubwa unategemewa kuwaka kutokana na umahiri wa warembo hawa wa kurusha makonde ulingoni.

Helen atakuwa anarudisha heshina yake baada ya kupoteza pambano la ubingwa wa dunia kwa mwanadada Dahianna Santana wa Dominican Republic mwezi wa Desemba mwaka jana. Hii ni heshima pekee kwa kina mama kutoka bara la Afrika wa kuonyesha umahiri wao kwa binti huyo wa Kifalme kutoka Hungary.
 
                                                          Albert Mensah (kulia)
Ndipo litakapokuja pambano la kukata na shoka kati ya mbabe kijana anayeinukia katika ulimwengu wa masumbwi nchini Ghaha na Afrika kwa ujumla bondia Issa Samir kutoka Ghana atakapopambana na mbabe kutoka kwenye jangwa la barafu la Siberia, bondia Robison Omsarashvili kutoka katika nchi ya Georgia ambayo ni moja ya nchi zilizokuwa kwenye Muungano wa Kishoshalisti wa Sovieti ya Urusi (USSR).

Ni nderemo na vifijo kwa Waghana na watu wote wa Afrika wakati mabondia hawa watakapo pambana kugombea mataji haya makubwa kabisa ya IBF na kuliwakilisha bara la Afrika katika ramani ya dunia.

Mapambano haya yanaandaliwa na kampuni ya GoldenMike Boxing Syndicate ya Accra, Ghana chini ya Henry Many-Spain na Michael Tetteh na yatafanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Accra (Accra International Conference Center) na yatasimamiwa na Rais wa IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati Mtanzania Onesmo Ngowi.

IMETOLEWA NA:
INTERNATIONAL BOXING FEDERATION AFRICA (IBF/AFRICA)
DAR ES SALAAM, TANZANIA

No comments:

Post a Comment