Tangazo

Pages

Thursday, December 27, 2012

IBF YAMPONGEZA BINGWA MPYA WA AFRIKA, GHUBA YA UAJEMI NA MASHARIKI YA KATI

TAARIFA KW AVYOMBO VYA HABARI

TAREHE 27/12/2012

Shirilisho la Ngumi la Kimataifa (IBF) limepongeza bingwa mpya wa uzito wa Super Middle katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki yaa Kati, Mtanzania Francis Cheka.

Katika barua yake aliyomtumia Francis Cheka ya tarehe 28/12/2012 Mwenyekiti wa kamati ya Ubingwa wa IBF/USBA Lindsey Tucker alisema "Tunachukua fursa hii kukutakia maisha na mafanikio mazuri kama bingwa wa IBF na kumhimiza kuishi kama bingwa". Cheka atatakiwa kutetea taji lake katika kipindi cha miezi sita kufikia mwezi wa 6 mwakani dhidi ya mpinzani ambaye ana rekodi ya mapambano yasiyopungua 15 na mengi awe ameyashinda hususan mapambano mawili ya mwisho.

Aidha IBF inampongeza bondia Chiotcha Chimwemwe kutoka Malawi kwa ushupavu wake na ushindani mzuri katika pambano hilo lililofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid katika jiji la Arusha tarehe 26 Desemba, 2012.


Imetolewa na:


Onesmo A.M. Ngowi
Rais
IBF/USBA Afrka, Ghuba ya Uajemi an Mashariki ya Kati



CHIOTCHA AONJA MACHUNGU YA CHEKA

Bondia kutoka Jamhuri ya watu wa Malawi Chiotcha Chimwemwe alionja machungu ya Mtanzania Francis Cheka katika mpambano wao uliopewa jina na “Vita vya Ziwa Nyasa” tarehe 26 Desemba 2012 siku ya Boxing Day jijini Arusha.

Ulikuwa ni mpambano wa mwaka ambao bondia Francis Cheka nusura aupoteze katika raundi ya pili wakati konde zito la kushoto la kapteni Usu kutoka katika jeshi la jamhuri ya watu wa Malawi, Chiotcha lilipompeleka chini na kuinuka kwa msaaada wa kamba za ulingo.

Konde hilo zito lilifungua mpasuko mkubwa katika paji la Cheka na hivyo kuleta wasiwasi kwa mashabiki zaidi ya elfu 10 waliofurika katika uwanja wa Sheikh Amri Abed kumshughudia Cheka akipambana kiume kwelikweli.

Raundi ya kwanza mpaka ya nne Chiotcha alikuwa anamiliki mpambano huo na makonde mazito ya mkono wake wa kushoto kwani anatumia staili ya South Paw inayomlazimu kutanguliza mbele mguu wa kulia.

Ni katika raundi ya sita ambako Cheka aliweza kubadilisha mwelekeo wa mpambano kwa kuanza kumwadhibu Chiotcha na makonde mazito ya kombinasheni yaliyomfanya Mmalawi huyo kumkumbatia bila mafanikio Mtanzania huyo asiyepigika.

Cheka aliwanyanyua mashabiki waliojaa uwanjani wakiongozwa na Mstahiki Meya wa jiji la Arusha, Mh. Gaudence Lyimo alipompiga bila huruma Chiotcha na kumlazimu refarii wa kimataifa wa mpambano huo Nemes Kavishe wa Tanzania kumwonya kutomshika Cheka kama vile anapigana mieleka.,

Juhudi za Chiotcha kujisalimisha kwa kumkumbatia Cheka hazikuzaa matunda kwani aliendelea kupewa mkong’oto na mwana huyo wa Kitanzania aliyejizolea sifa kemkem kwa kuwapiga wapinzani wake.

Mashabiki wengi walinyanyuka katika viti vyao katika raundi ya 12 ya lala salama wakati Cheka alipodhihirisha kweli ni bondia asiyepigika kwa kumpiga makonde mazito kichwani Chiotcha na kumfanya apepesuke kila mara.

Katika mchezo huo ulioandaliwa na kampuni ya Green Hills (T) Investment ya jijini Dar-Es-Salaam inayomilikiwa na bingwa wa zamani wa taifa Andrew George, mabondia wa mapambano ya utanguliizi walikuwa wa ngumi za ridhaa kutoka katika jiji la Arusha.

Mpambano huo ulisimamiwa na Rais wa IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati, Mtanzania Onesmo Ngowi akisaidiwa na Kamishna wa TPBC kutoka Jiji la Arusha bw. Roman Chuwa.

Refarii alikuwa Nemes Kavishe kutoka Tanzania wakati majaji walikuwa: Daudi Chikwanje kutoka Malawi, Boniface Wambura kutoka Tanzania na Galous Ligongo kutoka Tanzania.


Imetolewa na

Uongozi, TPBC

No comments:

Post a Comment