Tangazo

Pages

Friday, February 1, 2013

TUZO ZA WANAMICHEZO BORA WA MWAKA 2013 SASA KUFANYIKA APRIL 27


Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya Tuzo za Mwanamichezo bora wa TASWA, Haji Manara, akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, leo mchana, wakati wakitangaza kuhusu kusogezwa mbele kwa shughuli hiyo ya utaoji tuzo ambapo sasa hafla hiyo itafanyika April 27, 2013, ambapo pia alizungumzia kwa ujumla maandalizi hayo. Katikati ni Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando, (kulia) ni Mjumbe wa TASWA, Turo Chambo.
Baadhi ya waandishi wa Habari waliohudhuria mkutano huo, leo.
*********************************
TUZO za Wanamichezo Bora wa Tanzania wa mwaka 2012 zinazoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) zitafanyika Aprili 27 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Kamati inayoratibu tuzo hiyo ilifanya kikao chake cha kwanza Jumanne wiki hii, ambapo wajumbe wa kamati hiyo walikubaliana mambo mbalimbali ya kimsingi kuhakikisha tuzo zinakuwa na mvuto kama ilivyokuwa miaka iliyopita na pengine ziwe bora zaidi.
Kutokana na hali hiyo vyama vyote vya michezo vilivyosajiliwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), ambavyo vipo hai na vinaendesha mashindano vitaandikiwa barua kwa ajili ya kutoa mependekezo yao ya wanamichezo waliofanya vizuri kwa mwaka jana upande wa michezo yao na yawasilishwe kabla ya Februari 28, mwaka huu.
Tunaomba ieleweke kuwa vyama vitatoa mapendekezo na hivi sasa Kamati ya Tuzo inafanya mazungumzo na kampuni mbalimbali zinazohusika na mambo ya mawasiliano ili kuona namna zitakavyoshirikiana na wadau katika kuchambua majina hayo, ambapo kila chama kimetakiwa kiwasilishe majina matano ya wanamichezo wao kwa kila jinsia kama ni mchezo unaochezwa na jinsia mbili, lakini kama ni mchezo wa jinsia moja watatakiwa kuwasilisha majina matano ya jinsia husika tu.
Yapo marekebisho kadhaa yamefanyika ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya tuzo kutoka 36 za mwaka jana hadi kufikia 42 mwaka huu na idadi inaweza kuongezeka ama kupungua kulingana na sifa za wanamichezo ambazo vyama vitaleta.

Tunaomba wadau watupe ushirikiano wa kutosha katika jambo hili ili kuzifanya tuzo ziwe bora na kuhakikisha kila anayestahili kupata tuzo anazawadiwa kwa kuthamini kile alichokifanya, ambapo ukumbi utakapofanyika tuzo hizo utatangazwa hivi karibuni baada ya kukamilisha baadhi ya mambo.

Idadi ya michezo itakayopewa tuzo pamoja na aina nyingine ya tuzo zitakazotolewa ikiwemo Tuzo ya Heshima tutaendelea kujulishana kadri siku zitakavyokuwa zinasonga mbele. Washindi wa kila tuzo ndiyo mmojawapo ataibuka kuwa Mwanamichezo Bora wa Tanzania Mwaka 2012.
Dhamira ya kamati yangu ni kutaka kuhakikisha kuwa TASWA haikukosea kututeua na tutaleta wanammichezo sahihi na hatimaye kumpata yule bora ambaye ataungana na wengine waliopata kutwaa tuzo hiyo miaka ya nyuma.
Wanamichezo ambao wamepata kutwaa Tuzo ya Mwanamichezo Bora Mwaka wa Tanzania ni Samson Ramadhan (2006),  Martin Sulle (2007) na Mary Naali (2008) wote wakiwa wanariadha, wakati mwaka 2009 alikuwa Mwanaidi Hassan na mwaka 2010 alikuwa pia Mwanaidi Hassan ambaye ni mcheza netiboli na mwaka 2011 alikuwa mwanasoka Shomari Kapombe.

Haji Manara
Mwenyekiti Kamati ya Tuzo za TASWA
01/02/2013

No comments:

Post a Comment