Tangazo

Pages

Monday, September 22, 2014

MGM Grand ilivyotokea kuwa makao makuu ya ndondi

MGM Grand ilivyotokea kuwa makao makuu ya ndondi - 1
*Floyd Mayweather amepageuza kuwa nyumbani kwake
*Ni hoteli ya pili kwa ukubwa duniani, eneo kubwa USA
LAS VEGAS, Marekani
FLOYD Mayweather (zamani Floyd Joy Sinclai ) amepigana mara 12 mfululizo jijini Las Vegas na kati ya mapigano hayo, 10 ni katika Ukumbi wa MGM Grand Garden Arena.
Alirudiana hapo wikiendi iliyopita na raia wa Argentina, Marcos Maidana na kumshinda.
"Floyd anapopigana hapa mambo ni tofauti kabisa. Kuna miale ya umeme usiyoweza kusimulia. Kuandaa pambano kama hili ni muhimu, si tu kwa hoteli yetu lakini pia kwa jiji zima. Kuna matukio mengi makubwa, na yote ni muhimu kwetu lakini pambano la Mayweather linaacha alama yake hapa," anasema Rais wa Michezo na Matukio wa MGM, Richard Sturm.
MGM Grand ni hoteli ya pili kwa ukubwa duniani kwa idadi ya vyumba, na kwa maana ya eneo - migahawa, maeneo ya kupumzikia na kadhalika ndiyo kubwa zaidi kote nchini Marekani, ikifuatiwa na The Venetian.
MGM ilipoanzishwa 1993 ilikuwa ndiyo hoteli kubwa zaidi duniani.
Mayweather ameifanya Las Vegas kuwa nyumbani kwake, binafsi lakini pia katika tasnia ya ngumi na unaweza kumwona hapa mwaka mzima kwenye jengo kubwa lenye ghorofa 20, iwe mchana au usiku.
Kila pambano lake lina thamani ya walau dola milioni 100 kwa uchumi wa Las Vegas lakini pia kuna mapato mengine ya pauni milioni 11 yasiyohusiana na kamari za kutabiri bingwa hapa, na mamilioni hayo yanaingizwa kutokana na mapato ya kwenye migahawa, vyumba vya hoteli na mengineyo.
"Las Vegas ni Jiji la mwanga, kila kitu ni kizuri, hapa ndipo nilipoanzia tasnia ya ngumi na hapa ndipo itakapoishia. Ni moja ya sehemu nzuri zaidi nilizopata kuona duniani," anasema Mayweather.
Lakini si huyu tu anayependa hapa, wanamasumbwi wengi wamekuwa wakipigana hapa, na kama mtakumbuka tangu zamani pamekuwa kama kivutio kikubwa cha mabondia chini ya wadhamini maarufu.
Nyota wengine waliopigana katika jiji hili ni pamoja na Mohammed Ali, Sugar Ray Leonard hadi akina Mike Tyson , Oscar De La Hoya na wengine wengi ambao wamekuwa wakiziba ombwe mara tu linapotokezea, kuhakikisha burudani zinaendelea, pesa zinachumwa na raha zinapondwa.
Baada ya kushinda pambano lake la wikiendi iliyopita, Mayweather sasa anafikiria nani tena amwite hapo MGM.
Mayweather anayejulikana pia kama Pretty Boy ni Mmarekani mwenye umri wa miaka 37 na ambaye hadi sasa ana utajiri wa dola milioni 295, alizaliwa Grand Rapids, Michigan.
Katika muda wake wa kucheza ngumi za kulipwa, ameshinda mara sita ubingwa katika madaraja matano tofauti ya uzani, rekodi ambayo haikupata kuwekwa na bondia mwingine.
Madaraja hayo ni Super Featherweight, Lightweight, Junior Welterweight, Welterweight mara mbili na Super Welterweight. Hadi sasa ameshinda mapambano yake yote 47 ya ngumi za kulipwa; hajui kupoteza pambano ni nini.
Miongoni mwa mapambano hayo, 28 amewaponda wapinzani wake kwa Knockout (KO) na kwa kiasi kikubwa ni mmoja wa wanamichezo wanaolipwa zaidi duniani, kama si kwamba yupo juu ya wengine.
Licha ya kutokuwa na wadhamini wengi anaoingia nao mkataba ili kuvaa vifaa vyao au kuwatangazia bidhaa zao, kwa mwaka dili za aina hiyo zinamwingizia dola milioni 80 anapopambana.
New York ndiyo ilikuwa ikitamba zamani kama makao makuu ya ndondi za ulimwengu, kwani kwa miongo mingi hapo ndipo redio, baadaye televisheni zilijenga mvuto mkubwa sana kwa watu katika sayansi tamu ya kupigana makonde.
Rekodi zinaonesha kwamba, ndondi ndio mchezo wa kwanza kabisa kurushwa kwenye televisheni moja kwa moja na hapo ni wakati Willie Pep alipohifadhi taji lake kwa kumchapa Chalky Wright mwaka 1944.
Katika baadhi ya maeneo ndondi zilipigwa karibu kila wikiendi usiku, zikawa maarufu lakini zikiandamana na machafuko mitaani, vioo vya nyumba za makazi na maduka vikivunjwa na mashabiki wanazi.
Yanakumbukwa maeneo kama  Garden  na Eastern Parkway Arena pamoja na St. Nick's na Sunnyside Gardens. Kadhalika hatutasahau Gillette na Pabst Blue Ribbon ambamo mabondia walizichapa na kuna wakati mara tatu kwa wiki pangekuwa na mapigano.
The Gillette Cavalcade of Sports yalirushwa kutoka Madison Square Garden, na ilianza rasmi kitaifa kwenye kituo cha televisheni cha NBC mwaka 1946, kabla ya kuzoeleka, kupendeka na kuwa maarufu kila Ijumaa usiku ukumbini lakini pia kwenye televisheni. ITAENDELEA WIKI IJAYO.
CHANZO: GAZETI LA SPOTILEO

No comments:

Post a Comment