Tangazo

Pages

Tuesday, December 17, 2013

Riddick Bowe afika mwisho wa reli

*Mbwembwe zimeisha, sasa amefilisika

*Bondia aliyempiga Holyfield mara mbili

*Marafiki wamemkimbia, aishia kuomba

Na Mwandishi Wetu

BONDIA anapozipiga ulingoni hupata washabiki wengi lakini akishatoka ulingoni uwezekano mkubwa ni kuishia katika ukiwa.

Sifa zile za pale kando ya jukwaa, kutoka kwa wenzake na zaidi sana kwa wanawake wa maumbo na umri tofauti ni kitu cha muda mfupi tu, kwani akishapotewa na fedha kila mmoja anamwacha.

Tunamkumbuka sana bondia Riddick Bowe aliyekuwa akishikilia mkanda wa uzito wa juu duniani.

Huyu katika maisha yake ya ubondia alifanikiwa kukusanya jumla ya dola milioni 50, ambapo katika maisha yake ya ubondia alipigwa mara moja tu.

Bowe anashikilia rekodi kubwa duniani, akiwa ni bondia pekee aliyefanikiwa kumpiga Evander Holyfield katika mashindano mawili.

Bowe aliupata ubingwa wa dunia akiwa na umri mdogo tu wa miaka 24, akaanza kuingiza mamilioni ya dola chini ya mkanda wake na pia kupitia kampuni alizokuwa akizitangaza kama vile Fila.

Lakini Bowe baada ya kuwa ameng’aa duniani kote kwa uwezo mkubwa katika masumbwi, alikuja kushuka kwa kasi hadi kufikia mtu wa kutafuta maisha kwa kuomba na hata kutafuta wateja ili awauzie nakala za wasifu wake ili apate kuiona siku inayofuata. Alionekana akitafuta wateja kwa nguvu katika maeneo ya New Jersey?

Mwenyewe Bowe anakiri kwamba alitumia vibaya wakati wake wa mafanikio, ikiwa ni pamoja na kuwa kwenye makasri ya ghali, magari lakini pia kusaidia wanafamilia na marafiki, akifikiri kwamba fedha zile hazingeisha, kumbe zilikuwa kama maua yanayochanua na kunyauka.

Lakini pia anasema kwamba fedha zake zilitumiwa vibaya na wasaidizi wake aliowaamini, akidhani angebaki juu kama bendera, enzi hizo akiitwa ‘Sugar Man’. Aliiweka vyema rekodi yake kwa kutwaa ubingwa unaotambuliwa na BA, WBC na IBF mwaka 1992.

Huyu ni mtu aliyezaliwa Agosti 10, 1967 huko Brooklyn, New York akiwa mtoto wa 12 kati ya 13 wa familia yake.

Kule alikokuwa akiishi katika utoto wake, kitongoji cha Brownsville kilikithiri kwa ubovu wa miundombinu, kikifananishwa na mitaa ya mabanda isiyo na hadhi.

Simanzi ya maisha yake iliongezeka kwa kumpoteza kaka yake, Henry, aliyethibitika kuwa alipatwa na Upungufu wa Kinga Mwilini (Ukimwi), lakini pia dada yake Brenda alifariki dunia baada ya kushambuliwa wakati wa jaribio la ujambazi nyumbani kwao 1988.

Mwaka 1988, akiwa bondia wa ngumi za ridhaa mwenye umri wa miaka 17, Bowe alimtwanga kwa Knock Out (KO) James Smith ndani ya sekunde nne tu.

Alikuwa kwenye mashindano ya Olimpiki ya Seoul 1988 ambako alitwaa medali ya fedha na amepata kuwa mshindi mara nne jijini kwake, katika kile walichokiita New York Golden Gloves Championships kuanzia 1985 hadi 1988.

Alianza uchezaji wa kulipwa Machi 1989 ambapo alimpiga kwa KO Lionel Butler. Wahanga wake wengine wa KO ni pamoja na Bert Cooper, Tyrell Biggs, Bruce Seldon na Pierre Coetzer.

Bowe alikuja kumuoa rafiki na mpenzi wake wa siku nyingi tangu enzi za sekondari, na ndoa yao ilikuwa Aprili 27, 1988 na wamejaliwa kupata watoto watano.

Hata hivyo, baada ya miaka ya tuhuma na shutuma za kwamba alikuwa hawatendei haki mke wala watoto wake, aliachana na mkewe Mei 1998 baada ya mkewe kufungua shauri la talaka mahakamani.

Miezi mitano baada ya utengano wao, Bowe alikamatwa na baadaye akatiwa hatiani kwa makosa ya kuwateka mkewe wa zamani na watoto wake, akatupwa jela kwa miezi 17. Ni bahati mbaya kwamba tunavyozungumza, Bowe ni mmoja wa wanamichezo waliofanikiwa sana enzi zao lakini ambao kwa sasa wamefilisika.

Jina lake kamili ni Riddick Lamont Bowe, lakini ukiacha ‘Sugar Man’ alikuwa pia akijulikana kwa jina la utani la Big Daddy.

Bowe alistaafu mwaka 1996 lakini akaamua kurudi tena ulingoni 2004 alikokaa hadi 2008 alipoona mambo hayaendi vizuri kwake, akatundika glavu tena.

Mwaka mmoja baadaye habari zilizagaa kwamba Bowe alikuwa katika hali mbaya hivyo kwamba alikuwa ameanza hata kuuza mali zake.

Alikwenda mbali zaidi na kuuza hata vile alivyopewa kama zawadi au tuzo katika maisha yake ya ubondia.

Alikataa kupokea ushauri nasaha kuhusu hali yake ili labda iwezekane kupata msaada wa kunusuru mali zake na kumwezesha kuwa na kipato kwa maisha yake yaliyobakia.

Alifikia mahali pa kuuza hata glavu zake, ambazo wenzake huzitundika kwa heshima na kumbukumbu kwa watoto, wajukuu na kizazi kijacho.

Kadhalika alikuwa anajaribu kila awezavyo kuuza picha zake mbalimbali ili kupata fedha za kusogeza maisha.

Hadi anastaafu, inasemwa kwamba alikuwa katika hali ya utajiri wa dola 15,000,000, lakini watu wanasema kutokana na aina ya maisha aliyokuwa nayo, hata angekuwa na dola bilioni 15 bado angefilisika tu.

Kwamba alichotakiwa kufanya, na ambacho wenzake sasa wanashauriwa ni kuwekeza fedha wanazopata ili ziendelee kuzalisha badala ya kuziweka kwenye chungu na kuchukua noti moja baada ya nyingine.

Ni wazi kwamba kwa mtindo huo zitaisha, hasa baada ya bondia kuwa ameshaacha kucheza na hata kuzalisha chochote.

Atatarajia vipi kwamba fedha zile, hata ziwe nyingi kiasi gani zitabaki pale pale au zitaongezeka? Bowe amekuwa na kawaida ya kukaa kwenye kiti cha uvivu kwenye baa akisubiri watu wafike kumwona ili kumpatia chochote na hata kununua vile alivyokuwa anauza.

Ni bahati mbaya nyingine kwamba licha ya hali ya kuishiwa fedha aliyokuwa nayo, Bowe alijitumbukiza kwenye unywaji wa kileo uliopindukia.

Septemba mwaka huu, Bowe alikuwa jijini London katika ziara lakini alionesha uchovu wake pale mwanahabari alipokwenda kumsalimu.

Bowe alimuuliza iwapo alikuwa rafiki yake, kisha akamwomba ampe fedha. Mwandishi yule mwenye umri mdogo tu alipoonesha kusita, Bowe alisema alikuwa akitania tu.

Hata hivyo, maneno yake mengine yanatia simanzi kama haya aliyosema katika mahojiano jijini London mwezi mmoja tu uliopita: “Daima nashukuru kwa yote ubondia ulionipatia na sasa ni muda wangu wa kutoa kama kufundisha vijana … acha nisaidie vijana hawa, nizungumze nao na kuona wana nini.

“Unajua wengi wa vijana siku hizi wanachofanya ni uhuni mitaani, kupigana na hata kuumizana. Ni bora wakaweka visu chini, wakavaa glavu ili waone kama zinaweza kuwasaidia kwa maisha yao ya baadaye”.

Anaeleza kwamba alikuwa na bahati na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa akiwa kijana kwa sababu alikuwa na watu waliomtunza, akipewa kila kitu alichohitaji.

“Sikukosa nilichohitaji au kutaka, iwe ni glavu, viatu vya kuvaa wakati wa kupigana na mahitaji yote. Watu wengi waliniamini na walikuwa karibu yangu … walinijaribu, walinipa fursa kwa hiyo sikuwa mitaani kuwaibia watu. Ni Mungu tu anajua ningekuwa nafanya nini badala ya masumbwi yale ulingoni,” anasema.

Bowe sasa, anakosa ukaribu wa wadau hao, muda wake ulingoni umekwisha, hana tena uwezo wa kupigana, lakini pia fedha alizokusanya zimetoweka au amezimaliza, kwa hiyo hakuna anayejali tena, pengine kwa kutoona sababu.

*Imeandikwa kutoka vyanzo mbalimbali kwenye mtandao

.Chanzo gazeti la SPOTILEO
zaidi tembelea mtandao wa
http://superdboxingcoach.blogspot.com/
na kwa mahitaji mbali mbali ya dvd za mafunzo ya ngumi wasiliana na kocha kwa namba za simu

0713406938

No comments:

Post a Comment