Tangazo

Pages

Friday, March 9, 2012

CHAMA CHA NGUMI ZA KULIPWA NCHINI CHATAMBULIKA KIMATAIFA

Na Mwandishi Wetu

SHIRIKISHO la Dunia la ngumi za kulipwa  (WPBF) limempa hati ya kuwa mwakilishi wa Shirikisho hilo nchini Rais wa Shirikisho la ngumi za kulipwa nchini (TPBO).
Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari kwa mtandao na Rais wa TPBO  Yassin Abdala 'Ustadhi' ilisema kuwa Shirikisho hilo lenye makazi yake nchini Marekani limempa hati hiyo ambayo itamruhusu kutoa taarifa muhimu za jinsi mabondia wa ngumi za kulipwa wa Tanzania wanavyoingizwa katika viwango vya Shirikisho hilo.
Alisema, sambamba na hilo pia litawasaidia mabondia watanzania kuweza kupata nafasi ya kugombea mikanda ya Shirikisho hilo.
"Ni jambo zuri kwa mabondia watanzania kwani watakuwa wanajua kila kitu kuhusu viwango vyao kuingizwa katika Shirikisho hilo lakini pia kupata nafasi ya kuwania mikanda hiyo ambayo itamsaidi kutambulika Ulimwenguni," alisema.
Sambamba na hilo pia Ustadhi amempongeza Mpiga picha wa Kampuni ya Business Times Limited inayochapisha magazeti ya Majira, Spoti Starehe na Business time,pamoja na Jarida la Maisha, ambaye pia ni Kocha wa Kimataifa wa Mchezo wa Masumbwi, Rajabu Mhamila 'Super D' kwa mchango wake katika kuhakikisha anaukuza mchezo wa ngumi bila kubagua.
Alisema, Super D  amekuwa ni  msaada mkubwa sana katika kila maandalizi ya mchezo kwa kuwasaidia waandaaji ambao hupungukwa vifaa vinavyohusu mchezo hususan glovus na vifaa vingine.
Sambamba na hilo amekuwa akifuatilia mapambano ya ngumi popote pale hata mkoani ,na huku akiyaripoti yote yanayofanyika huko nje ya Dar es salaam kwa galama zake mwenyewe.
"TPBO tunayo macho yenye kuona na kuthamini michango ya watu wa aina yako hivyo tunakuahidi kukupatia cheti cha kuthamini mchango wako katika tasnia hii ya mchezo wa ngumi  katika wakati muafaka," alisema.
Aliongeza kuwa yapo mengi ya kumshukuru kwani pia ameakuwa akiwasaidia mabondia wa mikoani kwa kuwauzia vifaa vya mchezo kwa bei ndogo kuliko hata ile ya madukani , hivyo kuwawezesha mabondia hao kuwa na uwezo wa kumiliki vifaa vya ngumi kiurahisi.

No comments:

Post a Comment