TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Shirikisho la Ngumi la Kimataifa katika bara la Afrika (IBF) Onesmo Ngowi wa Tanzania ataongoza ujumbe mzito toka Afrika
na Mashariki ya Kati na Ghuba ya Uajemi katika mkutano wa 29 wa
Shirikisho la Ngumi la Kimataifa na Chama Cha Ngumi Cha Marekani
(IBF/USBA). Mkutano huo utafanyika katika jiji la Honolulu, kwenye jimbo
la Hawaii nchini Marekani alikozaliwa Rais wa sasa wa Marekani Barak
Obama.
Jimbo
la Hawaii linajulikana sana duniani kama jiji la starehe ambalo hupokea
watalii wengi sana duniani wanaokwenda kule kustarehe. Hawaii ni jimbo
lililoko Kaskazini mwa nchi ya Marekani likiwa karibu zaidi na bara la
Asia!
Ujumbe
wa Afrika na Mashariki ya Kati atakaoungoza Ngowi utajumuisha viongozi
na wanachama wa Shirikisho la IBF katika nchi za Afrika ya Kusini,
Botswana, Namibia, Uganda, Ghana, Cote D’Ivoire, Morocco, Tunisia, Dubai, Oman na Jordan.
Hii
ni mara ya kwanza kwa Onesmo Ngowi kuongoza ujumbe toka Afrika na
Mashariki ya Kati na Ghuba ya Uajemi kwani mara zote huwa anaongoza
ujumbe wa bara la Afrika katika mikutano ya IBF/USBA. Kuongezewa wigo wa
madaraka kwa Ngowi kumekuja wakati ambapo IBF/USBA inapanua wigo wa
shughuli zake katika masoko yanayoinukia hususan katika mataifa
yanayozalisha mafuta kwa wingi duniani.
Mashariki
ya Kati ni moja na sehemu zenye utajiri mkubwa sana duniani kutokana na
uzalishaji wake mkubwa wa mafuta na gesi. Nchi ya Dubai ambayo ni
kiungo kikubwa sana cha biashara za kimataifa ikiziunganisha Ulaya, Asia
na mataifa mengine ya Marekani, Afrika imeteuliwa na IBF kuwa ni kitovu
cha shughuli zake Mashariki ya Kati na Ghuba ya Uajemi.
Baadhi
ya wajumbe mashughuri watakaokuwa katika msafara huo na nchi zao kwenye
mabano ni pamoja na: Issac Tshabalala, Alfred Bugwane, Branco
Milenkovic (Afrika ya Kusini), Justin Juuko (Uganda), John Akaba (Cote
D’Ivoire), Skeikh Ahmed Omar (Morocco), Mohammed Hatimy (Tunisia) Sheikh
Khalifa Hassan, Mohammed Othman (Dubai), Yakub Yossef (Jordan), Julian
Homaulaba (Botswana), Michael Tetteh, Henry Mann-Spain (Ghana) na
Hussein Mohammed (Oman).
Katika
mkutano huo unaotarajiwa kuanza May 29 mpaka Juni 2, Ngowi atawasilisha
rasimu ya mradi wa IBF wa Utalii wa Michezo (IBF Sports Tourism) katika
kikao hicho baada ya kuteuliwa na mkutano wa mwaka jana uliofanyika
katika jiji la Las Vegas, liliko kwenye jimbo la Nevada nchini Marekani.
Katika kikao cha mwaka jana Ngowi alitakiwa kuja na rasimu ya mradi wa
IBF wa Utalii wa Michezo ambapo nchi za Tanzania na Ghana ziliteuliwa
kama nchi za majaribio katika bara la Afrika.
Kufanikiwa
kwa mradi huu kutaifanya Afrika hususan Tanzania kufaidi sana kutokana
na mtandao mpana wa IBF ambao uko katika nchi zaidi ya 203 duniani.
Katika mradi huu IBF wa Utalii wa Michezo wanachama wa IBF katika nchi
hizi watashawishiwa kuzitembelea Tanzania na Ghana kama watalii pamoja
na kuwekeza katika miradi mbalimbali.
Aidha
katika mradi huu IBF itafanya mikutano yake ya robo mwaka na mwaka
katika nchi za Tanzania na Ghana ikikuza utalii. Mikutano ya mwaka ya
IBF/USBSA huudhuriwa na watu zaidi ya 3000 toka nchi zaidi ya 203 kila
mwaka.
Imetolewa na,
Kitengo cha Mahusiano (PRO)
International Boxing Federation Africa (IBF/Africa)
Benjamin William Mkapa Pension Towers
Mezzanine Floor,
Dar-Es-Salaam - Tanzania
Tel: +255-754-360828
E-mail: ibfafrica@yahoo.com
Technology House, 35-38 Ghalla Road
P.O BOX 1106 MOSHI - TANZANIA
Tel/Fax: 255-27-2754743
Cell: +255-744-360828
E-mail: ibfafrica@yahoo.com
No comments:
Post a Comment