Tangazo

Pages

Tuesday, August 23, 2016

JIFUNZE MASUMBWI NA SUPER D COACH

ULINGO


SAFU hii inaendelea kuhusu sheria za mchezo wa ngumi, aina na staili za upiganaji na mambo mengi yanayouzunguka mchezo huu ambao unapendwa na wengi.
In-fighter/Swarmers
In-fighters/swarmers (wakati mwingine huitwa "pressure fighters") ni aina ya upiganaji ambapo bondia anakuwa hakai mbali na mpinzani wake, anakuwa ana kwa ana kila aendako.
Lakini jambo kubwa si kukaa ana kwa ana na mpinzani bali ni umahiri wao wa kurusha makombora mchanganyiko yaani ‘combinations’ hasa ‘hooks na uppercuts’.
Mpiganaji wa aina hii anahitaji kuwa mlinda kidevu chake mzuri kwani mara nyingi upiganaji huu hushambuliwa na ngumi ya mdonowo yaani ‘jab’ kabla ya wao kufanya kile wanachokusudia.
In-fighters hutumia staili hii ya upiganaji kwa kuwa wengi wao huwa ni wafupi kuliko wapinzani wao na hivyo kulazimika kupigana kwa makombora ya masafu mafupi na yenye kasi kupata ushindi.
Hata hivyo, baadhi ya mabondia warefu katika uzito mbalimbali wamekuwa pia wakipigana kwa staili hii, mfano ni Mike Tyson aliyewahi kuwa maarufu sana kwa ‘uppercuts’ zake zilizokuwa na madhara makubwa kwa wapinzani, pia Julio César Chávez, mabondia wengine ni Wayne McCullough, Amir Khan, Harry Greb, Jack Dempsey, Rocky Marciano, Joe Frazier, David Tua na Ricky Hatton.
Counter puncher
Counter punchers ni mabondia ‘wanaoteleza’ wenye kupigana kwa kujilinda zaidi na kutumia zaidi makosa ya mpinzani wake. Silaha yao kubwa ni kutumia makosa ya mpinzani na kuchukua pointi au hata kushinda kwa KO.
Hutumia muda mwingi kujikinga kuhakikisha wanazuia kila aina ya ngumi isiwapate na wakati huohuo kwa haraka kurusha makombora zaidi kwa kutegemea makosa ya mpinzani wake.
Mpinzani wake anaposhambulia yeye ndipo hupata mwanya wakati huohuo kulenga shabaha sehemu wazi iliyoachwa na mpinzani wake, kwa kuwa ni kawaida mtu anaposhambulia sehemu ya uso wake na nyingine huwa zinabaki wazi pasipokulindwa.
Hata hivyo, ili uwe mpiganaji wa staili hii, unapaswa kuwa na sifa zifuatazo. Uwe na mnyambuko (good reflexes), uwe mwenye kujaliwa akili ya upiganaji (intelligence), uwe na shabaha ya makonde (punch accuracy), lakini zaidi ya wepesi uwe  na mikono mwepesi yenye kasi ( good hand speed).
Baddhi ya mabondia katika kundi hili ni Jim Corbett, Jack Johnson, Laszlo Papp, Jerry Quarry, Anselmo Moreno, Chris Byrd, Bernard Hopkins, Vitali Klitschko, James Toney, Marvin Hagler, Evander Holyfield, Juan Manuel Márquez, Humberto Soto, Floyd Mayweather Jr, Roger Mayweather, Pernell Whitaker na  Max Schmeling.
·        Mchanganyiko wa staili
Mabondia wote duniani huwa na ujuzi wa msingi, ambapo kila bondia anapoanza ngumi hujikuta akitumia staili moja ambayo kwake inampa raha zaidi au inamfaa zaidi.
Lakini wanapokomaa katika fani hiyo lazima wawe na ujuzi wa zaidi ya staili hiyo waliyozoea ili wanapokutana na aina nyingine ya wapiganaji waweze kumudu pambano mfano, bondia wa staili ya ‘out-fighter’ atahitajika kutumia staili kukita miguu yake na kutumia staili ya ‘counter punch’, au kutumia mbimu za ‘slugger’ ili kuweza kumudu kupigana na bondia mwenye nguvu za mikono.
·        Staili dhidi ya staili
Je, kuna staili iliyo bora zaidi kuliko nyingine? Kinachokubalika na ambacho ni sahihi ni kwamba hakuna staili iliyo bora kuliko nyingine, zote zina faida yake na hasara yake lakini zaidi inategemea bondia mwenyewe anavyotumia staili yake isipokuwa kuna staili ambayo ina faida dhidi ya staili nyingine.
Mfano, mpiganaji wa staili ya ‘in-fighter’ ana faida anapopigana na mpiganaji wa ‘out-fighter’,  mpiganaji wa staili ya ‘out-fighter’ ana faida anapokutana na bondia wa staili ya ‘puncher’, bondia ‘puncher’ ana faida dhidi ya bondia ‘in-fighter’.
Huu ni mzunguko ambao unafanya kusiwepo na staili iliyo bora kuliko nyingine kwakua staili moja inaweza kuwa bora ya nyingine lakini ikawa dhaifu kwa nyingine.
Kwa asili sababu nyingine zinazochangia ubora wa staili husika ni kipaji, ujuzi na akili ya bondia mwenyewe pia aina ya mazoezi anayofanya na ndio maana kuna msemo kwamba staili hutengeneza upiganaji ("styles make fights"),
Ndiyo maana unakuta kwa mfano Joe Frazier alikuwa mzuri na kumsumbua sana Muhammad Ali, lakini alikuwa ‘nyanya’ kwa George Foreman ambaye naye alikuwa ‘nyanya’ kwa Ali.
**Mwandishi ni kocha wa mchezo wa ngumi anayefundisha klabu mbalimbali Dar es Salaam. Anapatikana kwa simu 0713/0787- 406938 au email: superdboxingcoach@gmail.com
 

No comments:

Post a Comment