Tangazo

Pages

Wednesday, April 6, 2016

Nike wanavyowatesa Maria Sharapova, Manny


Pacquiao
  NA MITANDAO
WANAMICHEZO wawili maarufu duniani, bondia Manny Pacquiao na mcheza tenisi, Maria Sharapova, wamejikuta wakipoteza mamilioni ya fedha walizokuwa wakiingiza kupitia udhamini wao baada ya kuingia matatani na wadhamini wao kwa mambo mawili tofauti.
Wakati Pacquiao ambaye ni mwanasiasa maarufu nchini kwao Ufilipino akijikuta matatani kutokana na kauli yake aliyoitoa hivi karibuni kwa kuwashambulia mashoha, Maria mapema wiki hii alilitia doa jina lake kutokana na kashfa ya kutumia dawa zilizokatazwa michezoni.
Katika maoni yake hayo dhidi ya mashoga aliyoyatoa wakati wa mahojiano na kituo cha televisheni cha Ufilipino, ambako anawania nafasi ya useneta kuelekea uchaguzi wa Mei mwaka huu, Pacquiao mwenye umri wa miaka 37, alisema: “Ni hali ya kawaida. Huwa unaona wanyama wa jinsia moja wakifanya ngono?
“Wanyama ni bora zaidi kwasababu wanaweza kutofautisha mwanamke na mwanaume. Iwapo mwanaume anafanya ngono na mwanaume mwenzake na mwanamke anashiriki tendo hilo la ngono na mwanamke mwenzake, ni wabaya zaidi ya wanyamya.”
Na akiwa anajiandaa kupanda ulingoni kwa mara ya mwisho dhidi ya Timothy Bradley Aprili 9, mwaka huu, bondia huyo amejikuta akipata pigo baada ya wadhamini wake, kampuni ya Nike kuvunja mkataba baina ya pande hizo mbili.
Nike walitoa taarifa yao huu ya uamuzi wao huo, iliyosomeka: “Tumebaini maoni ya Manny Pacquiao yamepingana na mawazo ya wengine.
“Nike tungapinga kwa nguvu zote ubaguzi wa aina yoyote na imekuwa na historia ndefu ya kusapoti kusimamia haki za jamii ya watu wenye uhusiano wa jinsia moja. Kuanzia sasa hatuna uhusiano wowote na Manny Pacquiao.”
Hata hivyo, Pacquiao aliomba msamaha uliotajwa kuwa dhaifu, akisema: “Samahani kwa kuwaumiza watu kwa kulinganisha mapenzi ya jinsi moja na wanyama. Niliowaumizi naomba wanisamehe tafadhali.
“Bado ninasimama katika imani yangu kuwa ninapingana na ndoa za jinsia moja kwasababu ya kile Biblia inachosema. Ninawapenda wote kwa mapenzi ya Mungu. Mungu awabariki wote na ninawaombea.”
Na anapojiandaa kushuka dimbani kwa mara ya mwisho, ni wazi kuwa kujitoa kwa wadhamini wake kutokana na maoni yake hayo dhidi ya mashoga, kutakuwa kumemwathiri kwa kiasi kikubwa katika suala zima la kimaslahi, lakini pia harakati zake za kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Ufilipino.
Kwa upande wake,  Maria Sharapova amejikuta kwenye hasara kubwa ya maisha yake baada ya kupoteza dili lake na Nike lenye thamani ya Dola za Marekani milioni 70 ndani ya saa moja tu baada ya kutangaza kuwa amekutwa ametumia dawa ambazo hazitakiwi kwa wanamichezo.
Maria amebainika kutumia dawa ambazo haziruhusiwi kwenye michezo ambazo amezitaja kama mildronate au meldonium kuanzia Januari mwaka huu baada ya kufanyiwa vipimo.
Baada ya habari hizo kutoka, wadhamini wake wakaanza kuvunja mikataba, kuanzia Nike ambao ndio walikua na dili kubwa la Dola hizo za Marekani milioni 70, kabla ya kampuni ya nembo za saa za mkononi za TAG Heuer nao kujitoa kumdhamini mwanadada huyo wa Urusi.
Msemaji wa Nike amesema: “Tumesitisha kufanya kazi na Sharapova kwa wakati huu tukiendelea na uchunguzi hadi hapo baadaye.”
Kutokana na takwimu za Forbes, Sharapova alikua akipokea Dola za Marekani milioni 30 kwa mwaka kutokana na mishahara mbalimbali na kwamba fedha hizo zinatarajiwa kushuka kutokana na wadhamini wake kuvunja mikataba.
Kwa upande mwingine, kitendo cha Nike kusitisha mikataba na wanamichezo hao, kimepokewa kwa hisia tofauti duniani kote, ikiwamo hapa Tanzania, baadhi wakiwasapoti, huku wengine wakiwashangaa kwa uamuzi wao huo wakidai umelenga katika kukomoana.
Mmoja wa wadau maarufu wa ndondi nchini Tanzania, Rajab Mhamila ‘Super D’, alisema: “Watu wengi wana hobi zao, Manny Pacquiao hajatoa maoni yake kwa kubuni tu, ametoa mistari katika Biblia kuwa hakuna mapenzi ya jinsia moja, kasimamia katika ukweli na uhakika, huwezi kupinga ukweli, inawezekana kuna watu ndani ya Nike hawajafurahishwa na maoni yake.
“Pacquiao ni mtu wa Mungu ndio maana hata katika mapambano yake lazima utamuona akiwa amevaa msalaba, anasimamia imani yake na ndio maana alitoa vifungu vya mistari katika utetezi wake akisema sisi binadamu tumekuwa wabaya zaidi ya wanyama ambao hawawezi kufanya vitendo hivyo wanavyofanya baadhi ya binadamu. Mimi nipo upande wa Pacquiao.”
Hata katika mitandao mbalimbali ya kijamii ya Tweeter, Instagram, facebook na mingineyo, wapo wachache mno waliosapoti uamuzi wa Nike dhidi ya Pacquiao na Maria, huku wengi wakionekana kuiponda kampuni hiyo kwa kukurupuka katika maamuzi yao, hasa kitendo cha kumtosa Pacquiao.

No comments:

Post a Comment