Tangazo

Pages

Thursday, January 22, 2015

ZAINABU ‘IKOTA’ MHAMILA Yoso wa masumbwi anayefuata nyayo za baba yake

Kocha wa kimataifa wa mchezo wa masumbwi nchini Rajabu Mhamila 'Super D' kushoto akimwelekeza jinsi ya kurusha makonde bondia Zainabu 'Ikota' Mhamila ambaye ni binti yake anaependa ngumi kwa ajili ya kujiweka fiti katika mazoezi picha na SUPER D BOXING NEWS
JANUARI 14, 2015 alikuwa akisherehekea miaka 13 tangu kuzaliwa kwake, lakini moja ya rekodi nzuri aliyonayo katika ulimwengu wa masumbwi, licha ya umri mdogo alionao ni pambano lake kurushwa ‘live’ runingani miaka mitatu iliyopita.
Pambano hilo alilicheza kwenye Ukumbi wa Panandi Panandi, akiwa na umri wa miaka 10 na kuoneshwa ‘live’ runingani kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1), wakati alipopanda ulingoni kuumana na rafiki yake mkubwa Zulfa Medese.
Hapa namzungumzia bondia chipukizi wa kike nchini, anayethibitisha usemi kuwa; Mtoto wa nyoka, ni nyoka, huyu ni Zainabu Mhamila maarufu kwa jina la Ikota, ambaye ni mtoto wa nguli na kocha wa kimataifa wa mchezo huo, Rajabu Mhamila ‘Super D.’
Katika mahojiano yaliyozaa makala hii, Ikota anakiri wazi kuupenda mchezo wa masumbwi kutokana na ukweli aliouita kuwa ‘masumbwi yako katika damu yake’ kutokana na kuzaliwa katika koo ya wanamasumbwi.
“Nimekulia katika mazingira ya mchezo huu, nadhani hii ndio sababu kuu ya kuupenda. Baba yangu mzazi (Super D) ni kocha wa ndondi na bondia wa zamani, lakini pia baba yangu mkubwa Shabani Mhamila ‘Star Boy ni mwanamasumbwi,” alisema Ikota.
Ikota anayefanya mazoezi yak echini ya ukufunzi wa baba yake Super D, anabainisha kuwa, ukiwaondoa Super D na Star Boy – (ambaye alikuwa bingwa wa Taifa mwaka 2004), mkali mwingine wa mchezo huo katika ukoo wao ni baba yake mdogo.
“Baba yangu mdogo Rashidi Mhamila ‘Nature Fire’ ni mkali pia wa mchezo huu, pamoja na ndugu yetu yetu mwingine Mohammed Hemedi Kidogo ‘Ninja.’ Huo ni uthibitisho kuwa masumbwi ni mchezo ulio kwenye damu yangu,” alisema Ikota.
 
Masomo na michezo kwa mpigo
 
Mwaka huu wa 2015 Ikota ni mwanafunzi wa darasa la saba, katika Shule ya Msingi Msimbazi Mseto, Ilala jijini Dar es Salaam, hii imemlazimu kupunguza ratiba ya ushiriki wake katika ndondi ili kujipa muda zaidi wa kusoma.
“Nimepunguziwa ratiba ya mazoezi na ushiriki wangu kwa ujumla na baba yangu, ili kunipa muda wa kutosha kujisomea kuelekea mitihani ya taifa ya darasa la saba, hivyo kwa sasa nimejikita zaidi katika elimu ili kutojiangusha,” anasema Ikota.
Kwa mujibu wa baba wa binti huyu, Super D, ni kwamba kiwango cha elimu cha Ikota hakijaathiriwa kamwe na ushiriki wake katika michezo na kwamba yuko katika uangalizi salama ambao hauhatarishi umakini wake shuleni.
 
Mabondia wa nje wanaomvutia
 
Ukiondoa mabondia waliojazana katika ukoo wake, Ikota anakiri wazi kuwazimia mabondia wengine wa nje ya nchi, akiwamo mwanamasumbwi anayechanganya na siasa na Mbunge wa Sarangani, Uphilipino, Emmanuel ‘Manny’ Dapidran Pacquiao.
“Lakini pia Ikota ni shabiki wa kutupwa wa bondia tajiri kuliko wananamichezo wote duniani, Floyd Joy Sinclair ambaye anatambulika zaidi kwa jina la Floyd Mayweather Jr,” anasema baba wa Ikota, Super D katika mahojiano haya pia.
 
Changamoto anayokabiliana nayo Ikota
 
Super D anakiri kuwa, changamoto kuu anayokutana na binti yake katika mchezo wa masumbwi ni uhaba wa mabondia chipukizi wa kike, hivyo kumkosesha changamoto ya kupima uwezo wake ulingoni kupitia mapambano ya kirafiki.
“Hata katika pambano lake lililorushwa ‘live’ TBC1, alicheza na rafiki yake Zulfa kutoka na uhaba wa chipukizi wa kike. Nitoe wito kwa wazazi kuwaruhusu mabinti kushiriki masumbwi na kuachana na fikra kuwa huu ni mchezo wa wanaume,” anasema Super D.
 
KWA UFUPI
JINA KAMILI: Zainabu Rajabu Mhamila ‘Ikota’
JINA LA BABA: Rajabu Mhamila ‘Super D’
JINA LA MAMA: Asha Kamnyanga ‘Mama Ikota’
KUZALIWA: Januari 14, 2003
ALIKOZALIWA: Amana Hospitali, Ilala
MCHEZO: Ngumi za Ridhaa
SHULE: Msimbazi Mseto, Ilala Dar
DARASA: La Saba ‘Std VII’
Kocha wa kimataifa wa mchezo wa masumbwi nchini Rajabu Mhamila 'Super D' kushoto akiwa na binti yake baada ya mazoezi

No comments:

Post a Comment