UNAPENDWA NA
KUOGOPWA NA WATU WENGI DUNIANI
UKO HATARINI
KUPOTEZA ASILI YAKE KABISA
Na Onesmo Ngowi
Masumbiwi au kwa majina mwengine
ndondi au ngumi na kwa majina ya mitaani ndogwa, mawe n.k. ni mchezo unapoendwa
sana na watu wengi. Aidha mchezo huu ni kati ya michezo inayoogopwa sana
duniani. Mchezo wa ngumi uko hatarini kupoteza maana yake ya asili yaani
kucheza kama burudani, kuwakilisha nchi na kujenga ushupavu wa mchezaji.
Mamilioni ya watu wanaojazana kuutazama wasingependa kabisa kujiingiza kuucheza
mchezo wa ngumi.
Japokuwa katika maisha ya
kawaida watu wengi hupigana kwa sababu mbalimbali kama vile kuwa na hasira,
kujilinda au kuwaonea tu wengine kwa sababu mbalimbali lakini kwa kawaida ni
watu wachache sana walio tayari kujiingiza katika kuucheza mchezo huu.
Kama tulivyokwisha ona kwenye
makala zilizotangulia, ngumi ni mchezo ambao ulianza wakati wanadamu walipoanza
tu kukunja ngumi na kurushina kama mchezo. Mchezo wa ngumi upo wa aina
mbalimbali.
Japokuwa kumbukumbu nyingi
zinaonyesha kwamba chimbuko haswa la mchezo huu linakubalika kuwa ni nchi za
kusini mwa Ulaya hususan Uyunani (leo Ugiriki) na Urumi (Italia ya leo) lakini
kuna mataifa au dola nyingine nyingi zilizokuwa na aina yao ya michezo
iliyofanana na ngumi. Wanazuoni wa
maswala ya michezo wanaifananisha michezo yote ya kupigana iwe ni kwa kutumia
mikono na miguu au kutumia silaha za aina mbalimbali na mchezo wa ngumi.
Aidha mchezo wa ngumi ni kati ya
michezo inayojenga ushupavu wa wachezaji na kuwafanya washujaa wa jamii.
Wachezaji wa ngumi mara nyingi ni watu wanaoonekana kama mashujaa kutokana na
ujasiri wanaoonyesha katika mchezo wenyewe.
Wakati wa utawala wa Marcus
Aurelius, mtawala shupavu wa iliyokuwa dola ya Roma (Italia ya leo) na aliyepata
mafanikio makubwa ya kuipanua dola ya Warumi (Italia) toka ukanda wa bahari ya
Mediterania hadi jangwa la barafu la Siberia huko Urusi, mashujaa wengi wa
michezo walichuana kwenye mashindano yaliyofanyika Coliseum (uwanja mkubwa
uliokuwa umejengwa katika jiji la Roma).
Mashujaa hawa ni pamoja na
wapiganaji ngumi na wengine walioshiriki kwenye michezo yenye hatari na
kujijengea umaarufu mkubwa kwenye jamii ya Warumi. Dola ya Warumi ilikuwa na
nguvu sana katika bara la Ulaya na ilienea hadi kaskazini mwa bara la Afrika.
Hivyo utamaduni wao hususan michezo iliyochezwa baada ya ushindi wa vita
ulienea kwenye himaya yao yote.
Kwa mfano katika dola ya
Manchuria (China ya leo) iliyotawala kutoka Uchina na nchi nyingi za mashariki
ya kusini mwa Asia ngumi zilijulikana kama Kung-Fu ambazo japokuwa kuchezwa kwa
ngumi hizi huchanganywa na mateke.
Maaskari wengi walitakiwa wawe
wamejifunza kupigana Kung Fu na waujue mchezo wenyewe kwa kiwango kikubwa. Kwao
Kung Fu ilikuwa ni aina nyingine ya silaha na walizitumia ipasavyo kwenye
kukabiliana na maadui kwenye vita. Baada
ya ushindi wa vita walikusanyika katika viwanja vikubwa na kucheza michezo hii
kama isahara ya kusheherekea ushindi wao.
Dola ya Kijapani iliyotawala
nchi nyingi za Asia ikiwa ni mpinzani mkubwa wa dola ya Manchuria katika karne
ya 12 nayo ilikuwa na mchezo wa ngumi uliojulikana kama Karate. Mashujaa wengi
wa Kijapani walitakiwa wawe na ujasiri wa hali ya juu wa kupigana Karate.
Kwao Karate ilikuwa sio mchezo
tu bali ni ufundi wa kumshinda adui kwenye vita. Ushindani mkubwa kati ya
Wachina na Wajapani uliifanya michezo ya Karate na Kung Fu kupata umaarufu
mkubwa sana. Kila upande uliuona mchezo wake kama bora kuliko mwingine.
Katika miaka ya karibuni watawa
wengi katika ukanda huu wanaojulikana kama Monks (monki) waiijifunza Karate na
Kung Fu kwa kiwango cha juu ili kujilinda na Maharamia waliokuwa wanawavamia na
kuiba mali zao.
Mtawala Genghis Khan wa dola ya
Mongolia (Mongol Empire) ambayo ilitawala kuanzia Mongolia yenyewe hadi Persia
(Irani), Babilon (Iraki) na baadhi ya nchi za Balkan (Ulaya ya Kati)
aliwachagua wapiganaji wake kwa ustadi na uangalifu mkubwa. Kwa kutumia
wapiganaji waliosheheni kila aina ya ushupavu aliweza kushinda majeshi mengi na
kuwa kati ya watawala walioogopewa sana wakati wa enzi yake.
Dola
ya Otoman ya Kituruki iliyotawala katika karne ya 19 ilitumia mchezo
ulioulikana sana na wengi kama Mieleka ukichanganya na utumiaji wa farasi. Mara
nyingi wachezaji wa mchezo huu walifariki kutokana na ugumu wa mchezo wenyewe
na watanzamaji walisisimka sana kuona damu ikimwagika. Kwao huu ulikuwa ndio
ushujaa tosha.
Nazo dola za Mafarao wa Misri
zilikuwa na aina yao ya michezo iliochezwa haswa na watumwa kwa minajili ya
kuwafurahisha Mafarao na familia zao hata katika kujitetea au kushambulia
maaduni! Kwa dhati kabisa mchezo wa ngumi ulivyojulikana na Wanafalsafa wa
zamani katika ukanda wa Mediterania katika dola nilizotaja hapo juu ulikuwa ni
mojawapo ya vipimo vya ujasiri wa mtu.
Sio
vibaya watanzania wakaelewa kuwa ngumi ni mchezo wa zamani sana kuchezwa hata
kabla nchi yetu haijatawaliwa na wakoloni katika karne ya 19. Michezo hii
iliyochezwa katika viwanja vikubwa vyenye mikusanyiko mikubwa ya watu
(Coliseum) huko Roma na (Arena) huko Athina, iliyokuwa katika hekalu kubwa la
ufalme wa Wayunani (Ugiriki) la Akropolis.
Viwanja hivi vilikuwa ndio
mwanzo wa ulingo wa kisasa kwani japokuwa ulingo wa kisasa ni wa mraba lakini
mwanzo wake ni Arena ya mduara.
Mwandishi
wa makala haya ni: Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC),
Shirkisho la Ngumi za Kulipwa Afrika Mashariki na Kati (ECAPBF), Shirikisho la
Ngumi la Kimataifa bara la Afrika (IBF/AFRICA) na Mkurugenzi wa Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola (CBC). E-mail: ibfafrica@yahoo.cm
No comments:
Post a Comment