ILIKUWA ni ndani ya ukumbi wa Hamburg, nchini Ujerumani usiku wa
kuamkia Oktoba 16,2010 pambano la kikatili lilipofanyika kwa kuwakutanisha
ndani ya ulingo bingwa wa WBC, Vitali Klitschko raia wa Ukraine aishiye
Ujerumani dhidi ya Shannon Briggs wa Marekani.
Utangulizi
Lilikuwa ni pambano la raundi 12, ambapo katika raundi zote hizo,
pambano lilikuwa likipiganwa kinyama bila huruma likiwa ni pambano la kuwania
ubngwa WBC uzani wa juu, huku Klitschko akitetea ubingwa wake kwa ushindi wa
pointi.
Raia huyo wa Ukraine pamoja na kutawala pambano hilo kwa raundi
zote akirusha ngumi nzito zilizotua kichwani kwa Mmarekani huyo, lakini
alishindwa kabisa kumkalisha chini kwa makonde.
“Nimeshangazwa sana namna alivyostahimili, nilimchapa makonde
mengi mazito na nimemchana lakini hakuanguka hata kidogo, Briggs anastahili
sifa,”anaeleza Klitschko baada ya
pambano hilo.
Katika pambano hilo, majaji wote walitoa alama 120-107, 120-107 na 120-105 kwa Klitschko, ambaye kwa ushindi
huo alijiwekea rekodi ya kushinda mapambano 41 akipigwa 2 wakati Briggs alivurunda rekodi yake na
kuwa 51-6-1.
“Nimepigana na George Foreman, nimepigana na Lennox Lewis, lakini
Vitali ni zaidi, alinipiga ngumi nzito sana ana kasi ya ajabu katika mikono yake,
kwangu mimi hili ni pambano bora,” anaeleza Briggs baada ya pambano hilo
Pambano ndani ya ulingo
Klitschko katika pambano hilo alikuwa akitumia ‘jab’ za kushoto
kumwinda Briggs kisha akawa anamaliza na ngumi kali ya kulia yaani ‘big right’.
Ndiivyo alivyoanza hivyo pambano hilo, alikuwa akimtupia jab ndani ya dakika
mbili za raundi ya kwanza kisha kuvurumisha konde kali la mkono wa kulia.
Kabla Briggs hajakaa sawa, akapigwa ‘left hooks’ mbili kidevuni
kisha M-Ukraine huyo akaachia fataki jingine la mkono wa kulia, Briggs akawa
anajaribu kujibu mashambulizi bila mfanikio.
Klitschko alikuwa akipiga ‘kombinesheni’ katika raundi ya tatu
lakini Briggs akawa anatumia ngumi za hesabu yaani ‘counter-punches’.
Klitschko alipiga ‘right hook’ safi mwishoni mwa raundi hiyo ya
tatu na akaendelea kutoa adhabu katika raundi ya nne.
Raundi ya tano, Briggs alijikakamua na kupiga ngumi kadhaa huku
akiendelea kupokea kipigo kikali kutoka kwa Klitschko.
Katika raundi ya 10, Briggs aligeuzwa kuwa begi la mazoezi ya
ngumi na Klitschko alikuwa
akichagua pa kupiga lakini alimshitukiza Klitschko alipoachia ngumi kali ya
kulia katika raundi ya 11,
lakini Klitschko akaibuka kwa ngumi mbili kali za kulia zilizofanya kichwa cha Briggs kuvimba kwa nyuma.
Lakini Briggs alishika kichwa na kugoma kabisa kupigwa KO na
kuendelea na pambano na hadi mwisho Klitschko akaambulia ushindi wa
pointi.
Shannon Briggs aliwahi kupigwa na George Foreman kabla ya
kudundwa na Lennox Lewis mwaka 1998.
**Mwandishi ni kocha wa
mchezo wa ngumi anayefundisha klabu mbalimbali Dar es Salaam. Anapatikana kwa
simu 0713/0787- 406938 au email: superdboxingcoach@gmail.com
No comments:
Post a Comment