Tangazo

Pages

Tuesday, August 23, 2016

James ‘Buster’ Douglas alianzia kwenye soka


LONDON, England 
JAMES ‘Buster’ Douglas aliushangaza ulimwengu wa masumbwi pale alipomtwanga bingwa aliyekuwa akichukuliwa kwamba hapigiki, Mike ‘Iron’ Tyson.
Pengine hiyo ndiyo rekodi kubwa zaidi inayokumbukwa na wafuatiliaji wa mchezo wa masumbwi.
Pambano hilo lilifanyika Tokyo, Japan 1990  na kwa sasa Douglas ameshastaafu na anakisiwa kuwa na utajiri wa jumla ya dola milioni tatu.
Douglas (53) ni Mmarekani aliyezaliwa Columbus jimbo la Ohio, na ni mtoto wa bondia wa zamani, William ‘Dynamite’ Douglas.
Amejijengea heshima kwa masumbwi yake mazito, lakini pia kwa nidhamu ndani na nje ya ulingo.
Mbali na ngumi, tangu utoto Douglas alipenda sana michezo mingine na shuleni Linden McKinley aliwika katika mchezo wa soka na wa kikapu.
Alikuwa mzuri kwenye mpira wa kikapu unaopendwa zaidi na Wamarekani hivyo kwamba aliwaongoza wana Linden kwenye michuano ya kitaifa 1977.
Baada ya hapo aliendeleza kipaji chake hicho kwa kucheza mpira wa kikapu alipokuwa Chuo cha Coffeyville kwa timu yao iliyojulikana kama Red Ravens iliyopo Coffeyville, Kansas kati ya 1977 na 1978.
Alikuwa akicheza kama fowadi na urefu wake wa futi sita na akaja kujumuishwa kama mwanamichezo bora wa timu ya Coffeyville.
Aliendelea na kikapu ambapo kati ya 1979 na 1980, Douglas alichezea Chuo cha Sinclair kilichopo Dayton, Ohio kabla ya kwenda Chuo Kikuu cha Mercyhurst kwa skolashipu ya kikapu.
Hata hivyo, baada ya muda aliamua kurudi Columbus alikojikita zaidi kwenye ngumi na awali alijulikana zaidi kwa jina la Dessert Fox.
Pambano lake la kwanza la ngumi lilikuwa Mei 31, 1981 alipopigana na kumshinda Dan O’Malley kwenye kipute cha raundi nne.
Je, aliwekaje historia kwa kumpiga Tyson? Lilipotangazwa pambano lao, karibu kila mdau aliona kwamba Tyson angeshinda kirahisi tena kwa Knock Out (KO).
Hata jijini Las Vegas, miongoni mwa wacheza kamari na watabiri wa ushindi wa kwenye masumbwi pale Mirage Casino ni mtu mmoja tu aliweka dau lake kwa Douglas kwamba angeshinda.
Siku ya siku ilipowadia Douglas alipanda ulingoni kwa kujiamini na utulivu mkubwa.
Tyson kama kawaida aliingia kwa makeke, akitishia kwa jinsi anavyotazama lakini hali haikumwendea vyema ulingoni kwa sababu alikipokea kichapo.
Douglas alishikilia mkanda huo wa uzani wa uu duniani kwa miezi minane na wiki mbili, akaja kuupoteza Oktoba 25, 1990 alipokuja kupigwa na Evander Holyfield kwa KO ya raundi ya tatu.
Katika ngumi kwa ujumla, Douglas amecheza mapambano 46, akashinda 38, kati ya hayo 24 kwa KO, akapoteza sita, sare moja na jingine likafutwa matokeo.
Baada ya muda wake kwenye ngumi kumalizika aliingia kwenye uigizaji wa filamu, akaanza na ile ya sayansi kwa Artie Knapp iliyoitwa Pluto’s Plight ambapo alikuwa nyota katika video hiyo.
Inaelezwa kwamba pambano la Douglas dhidi ya Holyfield liingiza dola milioni 24.6 lakini Douglas anasema kwamba alichpopata hapo ni dola milioni 1.5 tu.
Nyingine zilitumiwa kwa ajili ya kulipa kodi, mameneja, wakufunzi wake na mengineyo na anasema alipopigana na Tyson alipata dola milioni 1.3 lakini baada ya makato akabakiwa na dola 15,000 tu.
Douglas alikuja kuongezeka uzito kiasi cha kutisha na kufikia karibu pauni 400. Alikuja kupata kisukari akakisogelea kifo ndupo akaamua kujaribu kurejea kwenye michezo.
Alianza tena mazoezi na alipopangiwa mapambano alishinda sita ya kwanza mfululizo. Hata hivyo 1997 alipigwa isivyo halali na Louis Monaco ambaye alimtwanga ngumi nzito ya mkono wa kulia baada ya kengele ya raundi ya kwanza kumalizika kupigwa.
Hakuweza kuendelea na pambano hata baada ya kupumzishwa kwa dakika tano ambapo ngumi ile batili ilimrusha kwenye zulia.
Alipatiwa ushindi kwa majaji kumfutia pointi zote Monaco. Alikuja tena kucheza na Roy Jones, Jr mwishoni mwa miaka ya ’90 halafu akapigwa kwa KO na Lou Savarese kwenye raundi ya kwanza. Hakukata tamaa, akacheza tena mapambano mawili kabla ya kuamua kutundika glavu zake moja kwa moja 1999.

No comments:

Post a Comment