Tangazo

Pages

Tuesday, August 23, 2016

JIFUNZE MASUMBWI NA SUPER D COACH

(Ulingo)
Na Rajabu Mhamila ‘Super D’
 
Aina za upiganaji masumbwi
 
Vifaa vya kukinga mwili
KWAKUWA ngumi ni mchezo unaotumia nguvu, ni lazima tahadhari za hali ya juu zichukuliwe kuhakikisha mifupa katika kichwa na mikono vinalindwa, lakini pia ubongo na athari nyingine.
 
Makocha wengi huwa hawaruhusu mabondia wao kufanya mazoezi ya kupigana (sparring) bila kuvaa clip bandage (wrist wraps) na glavu.
 
(Hand wraps) hutumika kwa ajili ya kulinda mifupa katika mikono na kichwani, na glavu hutumika kukinga mifupa ya mikono kutojeruhiwa.
 
Glavu zimekuwa zikihitajika na kutumika na katika mashindano tangu karne ya 19 ijapokuwa glavu za ngumi za kisasa ni nzito kuliko zile za mwanzoni mwa karne ya 20.
 
Kabla ya pambano, mabondia wote hukubaliana ni glavu zenye uzito upi zitumike wakiwa na uelewa kwamba glavu inavyokuwa nyepesi ndivyo ngumi zinavyopenya zikiwa na athari zaidi na kuweza kusababisha madhara.
 
Bidhaa ya glavu pia huathiri ngumi kwa namna moja au nyingine ikitegemea glavu imetengenezwa na kampuni gani na imetengenezwa kwa kiwango gani na hivyo kabla ya pambano lazima kuwe na makubaliano ya glavu zitakazotumika.
 
Kipira cha mdomoni ni muhimu kukinga meno na fizi visijeruhiwe na pia kuifanya taya muda wote kuwa na tahadhari, unapokuwa na mouthpiece taya muda wote huwa linakakamaa kwa kuwa unauma kile kipira na hii inasaidia kupunguza nafasi ya kupigwa KO.
 
Mabondia wote wanatakiwa kuvaa soksi na viatu maalumu vya mchezo huo wa ngumi (ring boots), hii ni tahadhari ya kujikinga na ajali inayoweza kutokea kama kugongana au kukanyagana kwa bahati mbaya.
 
Viatu vya mabondia wa kale vilikuwa vinafanana na vya wanamieleka wa kale lakini vya sasa vinafanana na vya ngumi za ridhaa au mieleka ya ridhaa.
 
Vifaa vya mazoezi
Mabondia hujifunza ujuzi wa ngumi katika misingi miwili; ya begi la kufanyia mazoezi (punching bags). Begi dogo linaloitwa "speed bag" ambalo kazi yake kubwa ni kulainisha misuli na kufanya ngumi au mikono kuwa na kazi na begi kubwa "heavy bag"  ambalo hujazwa mchanga na pumba  au vitu vingine, kazi yake kubwa ni kukomaza mikono na kuifanya iwe na guvu.
 
Vifaa vingine ambavyo hutumika katika mchezo wa ngumi ni vifaa ambavyo si maalumu katika mchezo wa ngumi ilimradi vinajenga nguvu, kasi na stamina, vifaa vinavyojulikana katika mazoezi ni vitu vya kunyanyua uzito, kamba ya kuruka, ‘medicine balls’ na dumb bells’.
 
Staili na mbinu
Unaweza ukawa na staili ya upigaji kama niliyoeleza hapo juu lakini ukakosa mbinu na ndio maana ni muhimu bondia kuwa mjuvi katika mbinu na staili ambazo tutaziangalia kama ifuatavyo:
 
Mkao (Stance)
Mkao au stance ni namna bondia anavyosimama akiwa anapambana, unaweza kuwa na mbinu lakini pia staili. Kwa bondia yeyote duniani kuna aina kuu mbili za usimamaji.
 
Kutangulia mguu wa kushoto mbele (orthodox)
Hii ni staili au mkao au msimamo ambao unatumika kwa mabondia karibu wote wanaotumia mkono wa kulia katika matumizi ya kawaida ya kila siku katika maisha yao.
 
Mkao huu, bondia anatanguliza mguu wa kushoto mbele, anatumia ngumi ya kushoto kama ‘jab’ yaani ngumi mdonowo hivyo silaha yake ya ‘kumaliza mchezo’ inakuwa ni ngumi ya kulia, mkao huu unaitwa ‘Orthodox’, KO yake hutokea kwenye mkono wake wa kulia.
·        Kutangulia mguu wa kulia mbele (southpaw)
Hii ni staili au mkao au msimamo ambao unatumika kwa mabondia wachache sana ambao wengi wao hata katika maisha ya kila siku hutumia mkono wa kushoto.
Mkao huu, bondia anatanguliza mguu wa kulia mbele, anatumia ngumi ya kulia kama ngumi mdonowo ‘jab’, hivyo silaha yake ya ‘kumaliza mchezo’ inakuwa ni ngumi ya kushoto,  mkao huu unaitwa ‘Southpaw’. KO yake hutokea kwenye mkono wake wa kushoto.
 
Kwa upande wa nchi ya Cuba ambayo ilipiga marufuku mchezo wa ngumi za kulipwa, mabondia wake wote ni ‘southpaw, kwa hiyo si lazima bondia wa aina hii awe ni ‘mashoto’ (lefted hand) au orthodox awe lazima mtumia mkono wa kulia (right-handed).  
 
Kuanzia hapo staili nyingine au mikao midogo huwa imeegemea katika misingi ya mikao hiyo miwili mikubwa. Hata hivyo mikao ya sasa inatofautiana na mikao ya zamani ya karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20.
 
Misimamo au mikao ya sasa (modern stance) bondia anakuwa wima zaidi na mikono akiwa ameiweka mbele kidogo ya uso wake, au chini (low guard) tofauti na mikao ya zamani ambapo bondia alikuwa akisimama na mikono katanguliza mbele na nundu za ngumi (knuckles) zikiwa zimeelekea mbele.
 
Mikao hiyo ilitumika katika karne ya 20 na mfano mzuri ni bondia Jack Johnson, na hapa nitaelezea mikao hiyo yaani ‘stance’ kwa mifano ya picha kama ifuatavyo. Itaendelea wiki ijayo.
*Mwandishi ni kocha wa mchezo wa ngumi anayefundisha klabu mbalimbali za ngumi za kulipwa Dar es Salaam. Anapatikana kwa simu 0713/0787- 406938 au email: superdboxingcoach@gmail.com

No comments:

Post a Comment