Miyeyusho aliyemchakaza hivi karibuni Mzambia Fidelis Lupupa, alionyesha tangu mwanzoni mwa mchezo huo dhamira yake ya kuibuka ushindi, licha ya Momba kuonyesha upinzani mkubwa.
Wakiviziana na kudonoana kwa zamu, mabondia hao walijikuta wakimaliza pambano hilo la uzito wa bantam bila mashabiki kutabiri mapema nani mshindi kutokana na waliovyoonyesha upinzani katika mchezo huo.
Hata hivyo baada ya kumalizika kwa mchezo na majaji kutoa matokeo yao, mwamuzi Sako Mtilya alimtangaza Miyeyusho kuwa ndiye mshindi na kufanya mashabiki waliofurika kwenye ukumbi huo kumshangilia bondia huyo.
Huo ni ushindi wa 12 mfululizo kwa Miyeyusho ndani ya ardhi ya Tanzania tangu Aprili 2009 akiwapiga mabondia wa ndani na nje ya nchi.
Hata hivyo katika kipindi hicho, bondia huyo mwenye rekodi ya kucheza mapambano 47 na kushinda 36 akipoteza 10 na kuambulia sare mbili alishatoka nje ya nchi mara tatu na mara zote kudundwa na wapinzani wake kwa KO.
Katika pambano jingine la utangulizi Fadhili Awadh alimshinda kwa pointi Mussa Sunga katiika pambano lililokuwa limekaa ufundi.