Tangazo

Pages

Monday, September 29, 2014

BOXING FEATURE: KUELEKEA PAMBANO LA ALIBABA DHIDI YA THOAMS MASHALI OKTOBA 5


Allybaba Ramadhani

Masumbwi ni miongoni mwa michezo nchini Tanzania iliyowahi kuiletea nchi hii medali nyingi kutokana na umahiri wa watupa makonde kujituma vilivyo wawapo ulingoni katika mapambano yao.
Ninapozugumza hivi ninawakumbuka baadhi ya makocha na waliopo kwenye benchi kwenye mchezo wa soka wakati mwingine hutaka kurusha makonde pindi waonapo hali ni ngumu kwa timu zao.
Unamkumbuka kocha Jose Mourinho? kama sio sheria za FIFA kuwa kali angemtwanga kocha wa zamani wa Barcelona, marehemu Tito Vilanova aliyefariki mwaka huu kwa matatizo ya kansa akitoka kuachiwa mikoba na kocha wa sasa wa Bayern Munich, Pep Guardiola.
Mwingine ni German Burgos, kocha msaidizi wa Atletico Madrid akiwa na mtata mwenzake mwenye wenge la hatari, Diego Simeoni wote wakiwa waargentina waliotoka mbali lakini kwenye suala la kurusha ngumu hawajambo.
Unaweza kusema waache kufundisha soka waje, kipande hiki cha urushaji wa makonde, ha ha haaaa! Unacheka?
Hapa nchini tuna wanamasumbwi wengi ambao wamekuwa wakijitahidi kufanya mazoezi lakini hatma yao huwa ni kazi bure wafikapo katika medani ya kimataifa kutokana na mipango mibovu ya kuukuza mchezo huu.
Wapo mabondia wakali nchini wakitiwa moyo kama ilivyo katika soka wanaweza kuitangaza Tanzania kimataifa kwani hakuna kinachoshindikana.
Hata hivyo kuna madaraja ambayo mwanamasumbwi ni lazima apambane ili aweze kusonga hadi kujulikana kimataifa yakiwemo Superfeatherweight, Lightweight, Junior welterweight, welterweight, na Super welterweight.
Sijui kama watoto wetu wanajua haya!
Nchini Marekani miaka ya nyuma kabla ya mwaka 1950 kulitokea kizazi cha warusha mawe wa ukweli Willie Pep, Chalky Wright miaka ya 1944 na rekodi zinaonyesha mchezo huu ndio ulikuwa wa kwanza kurushwa moja kwa moja (live) katika luninga.
Walikuwepo George Foreman, Joe Frazier, na Muhammad Ali waliofanya vizuri katika medani hii na kulitangaza taifa la Marekani baada hapo kikaja kizazi cha kina Mike Tyson, Evander Holyfield na sasa ni kina Floyd  Mayweather.
Kimataifa zaidi wengineo ni Amir Khan, Manny Pacquiao, Marcos Maidana, Rocky Marciano na Oscar de la Hoya.
Leo, tutamwangazia bondia Alibaba Ramadhani wa mjini Moshi mkoani Kilimanjaro anayetarajiwa kutifuana na bondia Thomas Mashali wa Dar es Salaam hapo Jumapili Oktoba 5 mwaka huu katika pambano litakalofanyika Mkwakwani Mkoani Tanga.
HISTORIA YA ALIBABA RAMADHANI
Jina kamili anaitwa Alibaba Ramadhani (37), alizaliwa katika Hospitali ya Mawenzi mjini Moshi, mkoa Kilimanjaro t
arehe 23 Machi 1977.
Alianza elimu ya msingi mwaka 1984 na kuhitimu mwaka 1990 katika shule ya msingi Korongoni iliyopo Manispaa ya Moshi.
Mwaka 1991 aliingia kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Mlite iliyopo wilayani Rombo mkoni humu.
Hata hivyo hakufanikiwa kuhitimu elimu ya sekondari kwani mwaka 1992 alifukuzwa shuleni hapo kutokana na utovu wa nidhamu.
Baada ya hapo ajitupa katika shule ya ufundi na udereva mjini Moshi akisomea masuala ya ufundi makenika katika gereji moja ambako alifanikiwa kwa kiasi kikubwa katika fani hiyo.
Wakati akiendelea na mafunzo ya ufundi na udereva, Alibaba alijitumbukiza katika michezo mbalimbali ikiwemo utunishaji wa misuli kwa wanaume ambapo mwaka 1998 alishiriki shindano la kumtafuta Mr. Kilimanjaro na kumaliza nafasi ya 5.
Akiwa katika michezo mbalimbali ikiwemo kurusha tufe, mpira wa kikapu mwaka 1999 alikutana na Mwalimu Yasint ambaye alimshauri atinge CCP kwa ajili ya masumbwi.
Ndipo Oktoba 1999 alipoanza mazoezi makali, ilipofika Desemba 1999 alifuzu kushiriki michuano ya masumbwi kwa timu za majeshi yaliyofanyika CCP mjini Moshi na kuishia Nusu fainali.
Mpambano anaoukumbuka ni ule aliomchana sehemu ya jicho bondia Stanley Ernest katika raundi ya nne, hivyo kushinda kwa TKO hii ilikuwa mwaka 2000 na kutwaa mkanda wa mkoa.
Pia amewahi kupambana na Joshua Onyango mzaliwa wa Kenya anayeishi Marekani hii ilikuwa mwaka 2008, pambano hilo la kirafiki lilivunjika katika raundi ya tano.
Mwaka 2014 amepambana na Erick Mwenda katika ubingwa wa UBO-Africa raundi 10 na kumtwanga kwa pointi katika ukumbi wa YMCA mjini Moshi mapema mwezi Septemba mwaka huu.
Alibaba amepambana mapambano 22 akitoka sare pambano moja tu mengine akifanya vizuri.
BONDIA WA KIMATAIFA KIVUTIO
Akizungumza Alibaba alisema bondia Floyd Mayweather (37) wa nchini Marekani ndiye anayemvutia zaidi na hujisikia vizuri akimwona akishinda mapambano yake, hasa ikizingatiwa kwamba majuma machache yaliyopita amemtusua Muargentina Marcos Maidana.
KUELEKEA PAMBANO DHIDI YA THOMAS MASHALI
Wakali hawa watakuwa wakiwania mkanda wa UBO  Africa uzito wa kilogramu 72 .
Viunga vya mji wa Tanga vitarindima vigelegele na vifijo pale mabondia Ali Baba na Thomas Mashali watakapopanda ulingoni.
WITO KWA MABONDIA MAPROMOTA
Alibaba aliwataka mabondia wenzake  kufanya mazoezi na kuacha starehe na kujikita kufanya mazoezi kwa bidii zote ili kuurudisha mchezo huu kwenye zama zake.
Pia aliongeza kusema wanamasumbwi za zamani na wa kizazi cha sasa kuna utofauti mkubwa sana ikiwemo kupunguzwa kwa raundi kutoka 15 hadi kuwa chini ya 12 kutokana na wengi wao kukosa chakula cha kutosha na kujikita katika starehe badala ya mazoezi.
Hata hivyo Alibaba anayenolewa na Kocha Pascal Bruno kutoka Nairobi aliwataka mapromota wa mchezo kuacha tamaa ya fedha na badala yake wajikite kuwasaidia mabondia wao hali ambayo itaongeza hamasa kwa chipukizi.
WITO KWA SERIKALI
Aidha bondia huyo aliitaka serikali kuangazia mikoani na sio Dar es Salaam pekee kwani mikoani kuna wengi wenye uwezo wa kutosha hivyo mazingira yakiboreshwa yatasaidia kuinua mchezo huo kimataifa na kuachana na tabia ya kuwa wasindikizaji michuano mbalimbali.
Alibaba alihitimisha kwa kuwataka wakazi na wadau wa mkoa wa Kilimanjaro kuachana na dhana ya michezo hailipi na badala yake wawekeze katika m
chezo wa masumbwi badala ya kujikita katika masuala yasiyo ya kimichezo ili kuendeleza masumbwi.
Imetayarishwa na Jabir Johnson, barua pepe:jaizmela2010@gmail.com, cell: 0768 096 793

No comments:

Post a Comment