Tangazo

Pages

Thursday, March 27, 2014

Kaseba, Mashali nani kucheka Jumamosi?


* Wanawania mkanda wa UBO-Afrika
(PIX-Ngumi)
Kaseba, Mashali

BAADA ya tambo za muda mrefu kila moja akitamba kuwa ni zaidi ya mwenzake, mabondia Japhet Kaseba 'Champion' na Thomas  Mashali 'Simba Asiyefugika' wanatarajia kukata mzizi wa fitina mwishoni mwa wiki hii watakapopanda ulingoni kuzipiga.
Mabondia hao machachari wanaoshikilia ubingwa wa Taifa kila mmoja wa vyama 'hasimu' vya ngumi za kulipwa nchini, TPBO-Limited na PST watapanda ulingoni Machi 29 kwenye ukumbi waq PTA-Sabasaba jijini Dar es Salaam kuwania mkanda wa UBO-Afrika.
Pambano hilo litakalosindikizwa na michezo zaidi ya mitano ya utangulizi limeandaliwa na promota maarufu kutokea mjini Tanga, Ally Mwazoa chini ya usimamizi wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania (PST).
Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa mabondia hao kukutana ulingoni, huku kila mmoja akitamba kuwa ataibuka na ushindi kutokana na maandalizi waliyofanya kwenye kambi zao.
Mashali ambaye amepoteza mapambano mawili tu akipigwa na bingwa asiyepigika nchini, Francis Cheka na jingine la kimataifa dhidi ya Arif Magomedov wa Russia mwishoni mwa mwaka jana, ametamba kuwa Kaseba hana ubavu wa kumsimamisha kwa vile mpinzani wake huyo amelowea kwenye mchezo wa kick boxing.
"Tunamkaribisha kwenye ngumi na Machi 29 haitakuwa salama kwake kama alizoea kupigana na mabondia wepesi, safari hii anakutana na wakali wenyewe, asitarajie mteremko," alisema Mashali.
Mashali ametamba kuwa atamtia adabu mpinzani wake aliyewahi kuwa bingwa wa dunia wa kick boxing wa WCK na WKL kabla ya kurejea kwenye ngumi na kunyakua ubingwa wa PST dhidi ya Osward Maneno 'Mtambo wa Gongo'.
Hata hivyo Kaseba kwa upande wake aliliambia gazeti hili kuwa, amejiandaa kushinda pambano hilo ili kutwaa mkanda huo wa kimataifa ikiwa ni ndoto zake za muda mrefu.
"Kwanza nimefurahi kupata nafasi hii ya kuwania mkanda wa UBO Afrika, ni taji kubwa na nimekuwa na ndoto za muda mrefu za kunyakua mataji ya kimataifa baada ya kutamba kwenye kick boxing hivyo ni nafasi yangu," alisema
Kaseba, alisema ingawa hajajua atampiga Mashali katika raundi ya ngapi, lakini itakuwa ni mapema mno na kumtahadharisha mpinzani wake kuwa, ajiandae kupokea kipigo kwa sababu anataka kunyakua taji la kwanza la kimataifa baada ya kurejea katika ngumi.
Hata hivyo bondia huyo alikiri kwamba Mashali ni mmoja wa mabondia hodari na anamkubali kwa uwezo wake kwenye ulingo, lakini alisema amejipanga kumtandika ili kutimiza lengo lake la kutwaa taji hilo lililo wazi.
Mabondia hao wanakutana Jumamosi kila mmoja akiwa na rekodi yake, Kaseba anajivunia kucheza mapambano nane na kushinda matano, matatu yakiwa na KO na kupoteza matatu, huku mpinzani wake akiwa amecheza michezo 12 akishinda 9, mitano kwa KO na kupoteza mawili na kuambulia droo moja.
Mashali anayeshikilia pia ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati mara ya mwisho kupanda ulingoni ilikuwa Novemba mwaka jana nchini Russia na kupigwa kwa KO ya raundi ya pili dhidi ya Arif Magomedov wa Russia, huku Kaseba alishinda pambano lake la mwisho dhidi ya Alibaba Ramadhani baada ya kutoka kupokea kipigo cha KO ya raundi ya pili dhidi ya Jeremy van Diemen nchini Australia.
Hivyo kukutana kwao kwenye pambano hilo ni nafasi ya kila mmoja kutaka kuonyesha umahiri wake na kunyakua mkanda huo UBO.
Kuhusu maandalizi ya pambano hilo mratibu Ally Mwazoa alisema kila kitu kimekaa sawa na mashabiki wa ngumi wanapaswa kujitokeza ukumbini kupata uhondo kwani kutakuwa na mapambano matatu ya ubingwa, miwili ya kimataifa na mmoja wa Taifa-PST.
Mwazoa anayetokea mkoani Tanga, alisema mbali na pambano kuu la Kaseba na Mashali pia siku hiyo kutakuwa na pigano la kuwania ubingwa wa kimataifa wa UBO kati ya Allan Kamote dhidi ya Karage Suga katika uzito wa kilo 61.
Awali Kamote alikuwa amepangiwa kupigana na Fadhil Awadh ambaye alikumbwa na mauti siku chache baada ya kuugua ghafla na kukimbizwa Hospitali ya Mwananyamala alipokumbwa na mauti huku mkanda aliokuwa augombanie na Kamote ukiwa umetua nchini.
"Baada ya Awadh kufariki, Allan Kamote sasa atapambana na Karage Suba kuwania ubingwa wa Kimataifa wa UBO, pia siku hiyo kutakuwa na mchezo wa kuwania ubingwa wa taifa-PST kati ya Rajab Mhoja dhidi ya Fred Sayuni," alisema Mwazoa.
Mratibu huyo aliyataja mapambano mengine yatakayochezwa siuku hiyo ni pamoja na lile la  Haji Juma dhidi ya Juma Fundi, Zuberi Kitandula atakayepimana ubavu na Issa Omar na Baina Mazola dhidi ya Bakar Dunda.
Michezo mingine itawakutanisha Jumanne Mohammed atakayechapana na Shaaban Mtengela, wakongwe Said Chaku na Jocky Hamis wataonyeshana nao kazi na Majid atapimana ubavu dhidi ya Frank.
Mwazoa alisema wamejipanga katika kuhakikisha mashabiki watakaoenda ukumbini hapo kupata burudani bila bughudha kwa kuweka ulinzi madhubuti ukiongozwa na askari kanzu, kamera maalum na walinzi wengine shiriki ndani na nje ya ukumbi wa PTA.
"Tunafanya hivi kwa kutambua mabondia Kaseba na Mashali wana mashabiki wengi, tunashukuru Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Suleiman Kova ambaye ni Mlezi wa ngumi ametuhakikishia kila kitu kitakuwa sawa, hivyo mashabiki waje kwa wingi bila ya hofu," alisema Mwazoa.
Je, ni Japhet Kaseba au Thomas Mashali atakayecheka au kulia Jumamosi PTA? Tusubiri tuone.

No comments:

Post a Comment