MAUGO ADUNDWA NA CHEKA
BONDIA Francis Cheka ‘SMG’ kutoka Morogoro, kwa mara ya tatu
mfululizo Jana Usiku amempiga mpinzani wake Mada Maugo kwa Technical Knockout (TKO)
raundi ya saba katika pambano lililokuwa la raundi 12, kwenye ukumbi wa PTA,
Saba Saba, Dar es Salaam.
Maugo baada ya kupigwa ngumi nyingi katika raundi tatu
mfululizo, kiasi cha kutabiriwa kukaa chini wakati wowote, mwanzoni mwa raundi
ya saba hakurejea ulingoni.
Msaidizi wake, Karama Nyilawila alitupa taulo ulingoni akisema
bondia wake hataendelea na pambano.
Refa John Shipanuka kutoka Zambia aliyelimudu pambano hilo,
alimuinua mkono Cheka kumtangaza mshindi kwa TKO raundi ya saba.
Baada ya hapo, Maugo aliinuka kwenye kona yake na kwenda
kumkumbatia Cheka na kocha wake, akisema kwamba amesalimu amri baada ya kuishiwa
pumzi.
“Pumzi imekata, siwezi kuendelea,”alisema Maugo ambaye leo
alionekana muungwana ingawa hakuwa tayari kusema atahitaji pambano la nne au
la.
Akiwa mwenye furaha, Cheka alisema kwamba anamshukuru Mungu
amemuwezesha kuendeleza ubabe wake kwa mabondia wa Tanzania na sasa anageuzia
makali yake kwa Japhet Kaseba ambaye naye ameomba pambano la marudiano.
Katika pambano la jana, refa Shipanuka alimdhibitu Maugo
mwenye desturi ya kuwakumbatia wapinzani wake ili kukwepa kupigwa na pia kupumzikia
kwenye miili yao.
Kila alipokuwa akimkumbatia Cheka, Shipanuka alikuwa akifika
na kuwaachanisha na kufanya mabondia hao watumie muda mwingi kupigana.
Pamoja na hayo, Maugo alilianza pambano hilo vizuri na
katika raundi ya pili almanusra ashinde kwa Knockout (KO) baada ya kumkalisha
mpinzani wake kwa ngumi kali.
Lakini SMG aliinuka na kuendelea na pambano, ingawa
limchukua hadi raundi ya nne kuanza kuutawala mchezo.
Raundi ya kwanza hadi ya tatu, Maugo alifanya vizuri, lakini
baada ya hapo mambo yalikuwa magumu na tangu hapo wengi walijua angepigwa
wakati wowote.
Katika mapambano ya
utangulizi, mdogo wake Cheka, Cosmass Cheka alipigwa kwa pointi na Sadiki Momba
katika pambano la uzito wa Light, wakati Hajji Juma alimpiga kwa pointi Emmilio
Naffat uzito wa bantam.
Simba Watunduru alimpiga kwa KO raundi ya sita Mohamed
Kashinde katika pambano la uzito wa Feather, wakati Amos Mwamakala alimpiga kwa
pointi Said Muhiddin uzito wa Light.
No comments:
Post a Comment