Riddick Bowe afika mwisho wa reli
*Mbwembwe zimeisha, sasa amefilisika
*Bondia aliyempiga Holyfield mara mbili
*Marafiki wamemkimbia, aishia kuomba
Na Mwandishi Wetu
BONDIA anapozipiga ulingoni hupata washabiki wengi lakini akishatoka ulingoni uwezekano mkubwa ni kuishia katika ukiwa.
Sifa zile za pale kando ya jukwaa, kutoka kwa wenzake na zaidi sana kwa
wanawake wa maumbo na umri tofauti ni kitu cha muda mfupi tu, kwani
akishapotewa na fedha kila mmoja anamwacha.
Tunamkumbuka sana bondia Riddick Bowe aliyekuwa akishikilia mkanda wa uzito wa juu duniani.
Huyu katika maisha yake ya ubondia alifanikiwa kukusanya jumla ya dola
milioni 50, ambapo katika maisha yake ya ubondia alipigwa mara moja tu.
Bowe anashikilia rekodi kubwa duniani, akiwa ni bondia pekee aliyefanikiwa kumpiga Evander Holyfield katika mashindano mawili.
Bowe aliupata ubingwa wa dunia akiwa na umri mdogo tu wa miaka 24,
akaanza kuingiza mamilioni ya dola chini ya mkanda wake na pia kupitia
kampuni alizokuwa akizitangaza kama vile Fila.
Lakini Bowe
baada ya kuwa ameng’aa duniani kote kwa uwezo mkubwa katika masumbwi,
alikuja kushuka kwa kasi hadi kufikia mtu wa kutafuta maisha kwa kuomba
na hata kutafuta wateja ili awauzie nakala za wasifu wake ili apate
kuiona siku inayofuata. Alionekana akitafuta wateja kwa nguvu katika
maeneo ya New Jersey?
Mwenyewe Bowe anakiri kwamba alitumia
vibaya wakati wake wa mafanikio, ikiwa ni pamoja na kuwa kwenye makasri
ya ghali, magari lakini pia kusaidia wanafamilia na marafiki, akifikiri
kwamba fedha zile hazingeisha, kumbe zilikuwa kama maua yanayochanua na
kunyauka.
Lakini pia anasema kwamba fedha zake zilitumiwa
vibaya na wasaidizi wake aliowaamini, akidhani angebaki juu kama
bendera, enzi hizo akiitwa ‘Sugar Man’. Aliiweka vyema rekodi yake kwa
kutwaa ubingwa unaotambuliwa na BA, WBC na IBF mwaka 1992.
Huyu ni mtu aliyezaliwa Agosti 10, 1967 huko Brooklyn, New York akiwa mtoto wa 12 kati ya 13 wa familia yake.
Kule alikokuwa akiishi katika utoto wake, kitongoji cha Brownsville
kilikithiri kwa ubovu wa miundombinu, kikifananishwa na mitaa ya mabanda
isiyo na hadhi.
Simanzi ya maisha yake iliongezeka kwa
kumpoteza kaka yake, Henry, aliyethibitika kuwa alipatwa na Upungufu wa
Kinga Mwilini (Ukimwi), lakini pia dada yake Brenda alifariki dunia
baada ya kushambuliwa wakati wa jaribio la ujambazi nyumbani kwao 1988.
Mwaka 1988, akiwa bondia wa ngumi za ridhaa mwenye umri wa miaka 17,
Bowe alimtwanga kwa Knock Out (KO) James Smith ndani ya sekunde nne tu.
Alikuwa kwenye mashindano ya Olimpiki ya Seoul 1988 ambako alitwaa
medali ya fedha na amepata kuwa mshindi mara nne jijini kwake, katika
kile walichokiita New York Golden Gloves Championships kuanzia 1985 hadi
1988.
Alianza uchezaji wa kulipwa Machi 1989 ambapo alimpiga
kwa KO Lionel Butler. Wahanga wake wengine wa KO ni pamoja na Bert
Cooper, Tyrell Biggs, Bruce Seldon na Pierre Coetzer.
Bowe
alikuja kumuoa rafiki na mpenzi wake wa siku nyingi tangu enzi za
sekondari, na ndoa yao ilikuwa Aprili 27, 1988 na wamejaliwa kupata
watoto watano.
Hata hivyo, baada ya miaka ya tuhuma na shutuma
za kwamba alikuwa hawatendei haki mke wala watoto wake, aliachana na
mkewe Mei 1998 baada ya mkewe kufungua shauri la talaka mahakamani.
Miezi mitano baada ya utengano wao, Bowe alikamatwa na baadaye akatiwa
hatiani kwa makosa ya kuwateka mkewe wa zamani na watoto wake, akatupwa
jela kwa miezi 17. Ni bahati mbaya kwamba tunavyozungumza, Bowe ni mmoja
wa wanamichezo waliofanikiwa sana enzi zao lakini ambao kwa sasa
wamefilisika.
Jina lake kamili ni Riddick Lamont Bowe, lakini ukiacha ‘Sugar Man’ alikuwa pia akijulikana kwa jina la utani la Big Daddy.
Bowe alistaafu mwaka 1996 lakini akaamua kurudi tena ulingoni 2004
alikokaa hadi 2008 alipoona mambo hayaendi vizuri kwake, akatundika
glavu tena.
Mwaka mmoja baadaye habari zilizagaa kwamba Bowe alikuwa katika hali mbaya hivyo kwamba alikuwa ameanza hata kuuza mali zake.
Alikwenda mbali zaidi na kuuza hata vile alivyopewa kama zawadi au tuzo katika maisha yake ya ubondia.
Alikataa kupokea ushauri nasaha kuhusu hali yake ili labda iwezekane
kupata msaada wa kunusuru mali zake na kumwezesha kuwa na kipato kwa
maisha yake yaliyobakia.
Alifikia mahali pa kuuza hata glavu
zake, ambazo wenzake huzitundika kwa heshima na kumbukumbu kwa watoto,
wajukuu na kizazi kijacho.
Kadhalika alikuwa anajaribu kila awezavyo kuuza picha zake mbalimbali ili kupata fedha za kusogeza maisha.
Hadi anastaafu, inasemwa kwamba alikuwa katika hali ya utajiri wa dola
15,000,000, lakini watu wanasema kutokana na aina ya maisha aliyokuwa
nayo, hata angekuwa na dola bilioni 15 bado angefilisika tu.
Kwamba alichotakiwa kufanya, na ambacho wenzake sasa wanashauriwa ni
kuwekeza fedha wanazopata ili ziendelee kuzalisha badala ya kuziweka
kwenye chungu na kuchukua noti moja baada ya nyingine.
Ni wazi kwamba kwa mtindo huo zitaisha, hasa baada ya bondia kuwa ameshaacha kucheza na hata kuzalisha chochote.
Atatarajia vipi kwamba fedha zile, hata ziwe nyingi kiasi gani zitabaki
pale pale au zitaongezeka? Bowe amekuwa na kawaida ya kukaa kwenye kiti
cha uvivu kwenye baa akisubiri watu wafike kumwona ili kumpatia
chochote na hata kununua vile alivyokuwa anauza.
Ni bahati
mbaya nyingine kwamba licha ya hali ya kuishiwa fedha aliyokuwa nayo,
Bowe alijitumbukiza kwenye unywaji wa kileo uliopindukia.
Septemba mwaka huu, Bowe alikuwa jijini London katika ziara lakini
alionesha uchovu wake pale mwanahabari alipokwenda kumsalimu.
Bowe alimuuliza iwapo alikuwa rafiki yake, kisha akamwomba ampe fedha.
Mwandishi yule mwenye umri mdogo tu alipoonesha kusita, Bowe alisema
alikuwa akitania tu.
Hata hivyo, maneno yake mengine yanatia
simanzi kama haya aliyosema katika mahojiano jijini London mwezi mmoja
tu uliopita: “Daima nashukuru kwa yote ubondia ulionipatia na sasa ni
muda wangu wa kutoa kama kufundisha vijana … acha nisaidie vijana hawa,
nizungumze nao na kuona wana nini.
“Unajua wengi wa vijana
siku hizi wanachofanya ni uhuni mitaani, kupigana na hata kuumizana. Ni
bora wakaweka visu chini, wakavaa glavu ili waone kama zinaweza
kuwasaidia kwa maisha yao ya baadaye”.
Anaeleza kwamba alikuwa
na bahati na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa akiwa kijana kwa sababu
alikuwa na watu waliomtunza, akipewa kila kitu alichohitaji.
“Sikukosa nilichohitaji au kutaka, iwe ni glavu, viatu vya kuvaa wakati
wa kupigana na mahitaji yote. Watu wengi waliniamini na walikuwa karibu
yangu … walinijaribu, walinipa fursa kwa hiyo sikuwa mitaani kuwaibia
watu. Ni Mungu tu anajua ningekuwa nafanya nini badala ya masumbwi yale
ulingoni,” anasema.
Bowe sasa, anakosa ukaribu wa wadau hao,
muda wake ulingoni umekwisha, hana tena uwezo wa kupigana, lakini pia
fedha alizokusanya zimetoweka au amezimaliza, kwa hiyo hakuna anayejali
tena, pengine kwa kutoona sababu.
*Imeandikwa kutoka vyanzo mbalimbali kwenye mtandao
.Chanzo gazeti la SPOTILEO
zaidi tembelea mtandao wa
http://superdboxingcoach.blogspot.com/
na kwa mahitaji mbali mbali ya dvd za mafunzo ya ngumi wasiliana na kocha kwa namba za simu
0713406938
No comments:
Post a Comment