Tangazo

Pages

Tuesday, December 17, 2013

Frank Bruno: Maisha nje ya ulingo ni hatari kwake




Na Mwandishi Wetu
FRANKLIN Roy Bruno ndilo jina lake kamili, lakini kwenye ulingo wa masumbwi alizoeleka kama Frank Bruno.
Amefikisha umri wa miaka 50, kubwa la mafanikio kwake ni kutwaa ubingwa wa ngumi wa dunia unaoandaliwa na Baraza la Ngumi Duniani (WBC). Katika mapambano yake 45, ameshinda 40, kati ya hayo 38 KnockOut (KO) na kushindwa matano.
Mwingereza huyu aliyekulia Wandsworth, kusini mwa London baada ya wazazi wake kuhamia kutoka Caribbean, amekuja kukabiliana na magumu mengi baada ya kustaafu ngumi.
Imekuwa kama maruhani, maana alikumbwa na hali ambayo majirani walilazimika kuita polisi, wakamkamata na kumpeleka hospitali.
Hakuwa tena Bruno yule mstaarabu nje ya ulingo, bali alijaribu kuwa yule wa ulingoni, japokuwa alichokuwa akifanya hakikukamilika, na pengine kilikuwa hatari kwa afya yake.
Masahibu yalimwanza baada ya kustaafu ngumi rasmi 1996, akahangaika kuzoea maisha nje ya ulingo lakini wapi.Kuvunjika kwa ndoa yake na Laura mwaka 2001 kuliongeza msongo wa mawazo na mkanganyiko kimaisha.
Kilichoanza kuwa kama kawaida kwake, ilikuwa kulala kwenye ulingo aliotengeneza nyuma ya bustani nyumbani kwake, bila kujali hatari ya baridi kali kiafya, na wakati mwingine mvua.
Angekuwa kimya labda watu hawangeshituka, lakini alianza kuzunguka maili kadhaa nje ya mtaa wake akiwa peku miguuni, mdomoni akiwa ameweka gumshield wanayotumia wanamasumbwi kama ngao dhidi ya meno yao wanapopigana.
Wakati akizunguka bila mpangilio na katika hali ya kuvuruga utaratibu wa maisha wa watu wengine, Bruno alikuwa akijinasibu kwa kuwaambia watu yeye ni mpanda farasi, Frankie Dettori, Mtaliano aliyetwaa ubingwa wa mbio za farasi mara kadhaa.
Bruno alikuja kugeuka kero kwa majirani na watu wengine alikokatiza na kelele zake, akionekana kuwa na matatizo ya akili.
Hata hivyo aliachwa hadi 2003 ndipo kipenga kikapulizwa, kwa majirani kutoa taarifa kwa ndugu, ambao walilazimika kuita polisi waliomkamata na kumpeleka hospitali ya vichaa.
Bingwa huyo wa masumbwi aliyepata kudundana na Mike Tyson ulingoni, alipinga kwa nguvu zote kufungwa kamba na kuwekwa chini ya ulinzi hospitali, lakini hakufua dafu, sheria ikachukua mkondo wake.
Huko hospitalini alipata dawa na uangalizi kutoka kwa madaktari na wauguzi waliobobea, akaonekana kurejea hali yake nzuri ya awali, akaruhusiwa kurudi nyumbani.
Hata hivyo, tatizo la akili yake kutofanya kazi sawa lilionekana kuwa la kujirudia, maana haukupita muda akarudi tena kwenye mambo ya kulala ulingoni nje na kuranda mitaani akipiga kelele.
Bruno ambaye siku hizi anaonekana kuendelea vyema, bado anaeleza kuchukizwa na kukamatwa na kupelekwa hospitalini bila ridhaa yake.
“Ugonjwa wa akili unaweza kutokea kwa yeyote, hivyo nimeamua leo kusema haya. Wala haikutakiwa nikamatwe vile, nilihitaji msaada muda mrefu uliopita...watu wasione haya kuwa wazi pale wanapohitaji msaada,” anasema Bruno.
Mwaka jana mauzauza hayo yalimtokea tena Bruno, akakamatwa, kufungwa na kupelekwa hospitali ambako mwenyewe anasema ni afadhali kuwa gerezani kuliko hospitali.
Siku chache baada ya kuruhusiwa tena kutoka hospitali, Bruno anasimulia baadhi ya aliyokumbana nayo huko.
Moja ni mgonjwa mwenzake aliyeingia jikoni katika hospitali ya magonjwa ya akili ya Basildon, Essex, akachukua kisu kikubwa na kuanza kumsogelea. Anasema alipatwa taharuki kubwa lakini ikapishwa mbali.
“Nilikuwa nimekaa chumba cha maakuli, nikaona kijana aliyechukua kisu jikoni akinijia, lakini mara mlinzi alimkwida na kumwondoa.
Baada ya kuachiwa kutoka hospitali alikozuiliwa miezi kadhaa, Bruno aliamua kubadili mazingira kwa kusafiri na rafikiye wa kike, Nina Coletta.
Haukupita mwezi mmoja baada ya kurejea, alipata ugeni, kufumba na kufumbua kumbe ni maofisa wa polisi, waliompeleka Hospitali ya Mtakatifu Andrew iliyopo Nothampton, na huko alitulizwa kwa wiki tano.
Bruno anasema hapendi kutumia dawa kama mgonjwa, hivyo aliamua kutumia vifaa vya mazoezi kurejesha afya yake njema.
Katika umri wake wa miaka 50 leo, Bruno hufanya mazoezi magumu ya kulala kwa mgongo na kuamka (sit-ups) mara 4,000 kwa siku na pia hushiriki mbio ndefu.
Kwa sasa Bruno anaangaliwa na madaktari wa jamii, lakini anasema amedhamiria matatizo ya afya ya akili yasimrudie tena.
“Hili linaweza kuwa pambano langu gumu zaidi maishani – lakini nitafanya kila ninaloweza kulishinda,” anasema Bruno anayeonesha kujiamini.
Akiingia tu hapo, majirani ambao hawaamini kama mtu aina ya Bruno angefika maeneo yao, huanza kutuma ujumbe kwenye Twitter.
“Watu wa Glasgow ni wema na wananichukulia vizuri.hunisimamisha na kuniambia; ‘salamu bwana mkubwa’ napapenda kule, lakini si nyumbani kwangu – nyumbani ni hapa (Bedfordshire) na daima patabaki hivyo.”
“Raha yangu ni mazoezi, ni muhimu sana kwangu. Watu wengine hutumia muda kama huo kwenda baa kunywa au kuchukua mbwa na kutembea mitaani.
“Mie ni mazoezi tu, ndiyo njia ya kuacha shinikizo liondoke na kutulia. Wakati mwingine unajihisi kuwa na hasira sana kana kwamba si wewe. Nataka kuongeza mazoezi ili yaniondolee matatizo na kuniweka kwenye mstari,” anasema.
Kipaumbele chake sasa ni kuhakikisha kila siku anajihisi vyema viungo na akilini ili asipelekwe hospitali tena.
Hutembelewa kila mwezi na madaktari kwa ajili ya kumtazama nyumbani kwake, Bedfordshire, ambapo hudungwa sindano yenye nguvu kumzuia kurukwa akili.
“Nafanya kila madaktari wanachoniambia. Napata sindano na kufanya kila ninachoambiwa. Si vizuri kufikia hatua ya kukamatwa na kupelekwa hospitali. “Nilikwenda sehemu mbaya ajabu, ilikuwa kama jehanamu, sitaki kurudi tena kule,” anasema kwa simanzi.
*Makala haya yameandaliwa kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya habari.

Chanzo gazeti la SPOTILEO
zaidi tembelea mtandao wa
http://superdboxingcoach.blogspot.com/
na kwa mahitaji mbali mbali ya dvd za mafunzo ya ngumi wasiliana na kochwa kwa namba za simu

0713406938
DVD za mafunzo ya mchezo wa ngumi  kali pamoja na kutambua sheria zake zikiwa na mabondia wakali kama vile
Manny Paquaio, Saul 'canelo' alverez ,Floyd Mayweathar,Mike Tyson,Mohamed Ali,Ferex Trinidad,Miguel Cotto na wengine wengi
pia kuta kuwa na vifaa vya mchezo huo

No comments:

Post a Comment