 |
Rashid Matumla 'Snake Man' |
 |
Benson Mwakyembe |
 |
Karama Nyilawila aliyetwaa ubingwa wa WBF Ulaya |
MABONDIA Mada Maugo na Benson Mwakyembe Jumamosi walipokea vipigo nchini
Russia katika mapambano yao ya kimataifa, huku kukiwa na tuhuma kwamba
mabondia wengi wa Kitanzania wanaoenda kupigana nje ya nchi 'huuza'
mechi zao.
Maugo alipokea kichapo cha TKO ya raundi ya 5 katika
pambano la raundi 8 dhidi ya bondia asiye na uzoefu Movsur Yusupov
aliyecheza mapambano manne tu kulinganisha na Mtanzania huyo aliyepigana
michezo 25.
Mtanzania mwingine, Mwakyembe alidundwa kwa KO ya raundi
ya 7 ya pambano lake la raundi 8 dhidi ya bondia mwingine asiye na
uzoefu Apti Ustarkhanov, ambaye hilo lilikuwa ni pambano lake la tatu na
la pili kushinda tangu aingie kwenye ngumi za kulipwa.
Kina Maugo
walipambana dhidi ya wenyeji wao katika mapambano ya uzito wa Super
Middle ya raundi nane yaliyofanyika katika ukumbi wa Trade &
Entertainment Centre 'Moskva', Kaspiysk chini ya wakala Mkenya Thomas
Mutua.
Vipigo vya mabondia hao vimekuja wakati wadau wa ngumi za
kulipwa wakihoji sababu zinazofanya mabondia wa Kitanzania kushindwa
kutamba kila waendapo nje huku ripoti mbalimbali zikiwatuhumu mabondia
wa majuu kuwatumia mabondia kutoka Afrika kupandisha chati zao katika
viwango vya ubora kwa kuwanunua wawaachie washinde.
Ripoti za kuuzwa
mechi au kuwapo kwa mchezo mchafu ziliwahi kutolewa na baadhi ya
mabondia akiwamo Pascal Ndomba na Francis Cheka aliyepokea kichapo cha
kushangaza mapema mwaka huu nchini Ujerumani.
Ndomba anayepigana uzito wa juu wa (Cruiserweight), alisema baadhi
ya mawakala wa nje hutaka mabondia dhaifu wa kwenda kupigana na mabondia
wao ili kupata ushindi kirahisi na kuboresha rekodi zao.
"Hili ndilo
linalofanyika, bondia mkali mara chache sana kupelekwa nje na hata
akienda basi atahujumiwa ili apoteze mchezo kwa manufaa ya mabondia
wanaoenda kupigana nao," Ndomba alisema hivi karibuni.
Naye Cheka
alitoa maelezo ya kufanyiwa 'hila' katika pambano lake dhidi ya Uensal
Arik aliloongoza kwa raundi sita za mwanzo kabla ya kurushiwa kitaulo
katika raundi ya saba na kupoteza mchezo kwa TKO.
 |
Pascal Ndomba |
"Sikupoteza pambano lile, ila mwenyeji alibebwa na mwamuzi aliyemaliza
pambano kana kwamba nimesalimu amri, ni vigumu mabondia wa Tanzania
kushinda nje," alisema Cheka mara alipotua nchini.
Cheka alisema
kambi ya mpinzani wake walimfuata hadi hotelini alipofikia kuelekea
pambano lao kumshawishi awaachie pambano hilo kwa ahadi ya pesa lakini
alipokataa ndipo alipokuja kuhujumiwa ulingoni kwa mtu aliyekuwa upande
wa kona yake kurusha taulo ulingoni ilhali alikuwa akiongoza kwa pointi.
Bondia
huyo anayeaminika kuwa bora zaidi nchini kwa sasa katika uzito wake,
alisema hakuambatana na kocha wake wakati akienda katika pambano hilo
hivyo hata kwenye kona yake walikuwa wenyeji wake na ndiyo waliorusha
taulo ulingoni.
Hata hivyo, wapo waliomtuhumu kwamba huenda Cheka
alicheza 'dili' na wakala wa pambano hilo ili kutotibua rekodi ya
mpinzani wake ambaye alikuwa amepoteza pambano moja tu ya 18 aliyokuwa
amecheza.
NIPASHE ilizungumza na Marais wa Mashirikisho ya Ngumi za
Kulipwa Tanzania, Emmanuel Mlundwa wa PST na Yasin Abdallah 'Ustaadh' wa
TPBO kutaka kujua ukweli kuhusu tuhuma hizo, ambapo walikuwa na maoni
tofauti .
Mlundwa alisema kinachowaponza mabondia wa Tanzania siyo
hujuma wala nini ila maandalizi duni wanayofanya kabla ya mapambano yao
pia kuwa na viwango duni kulinganisha na wapinzani wao wanaoenda kucheza
nao.
"Ngumi za kulipwa ni biashara, mabondia wa ngumi hizo wanapotafutiwa
mechi wanapaswa kujiandaa, lakini hilo halifanyiki na hivyo kwenda
kulitia aibu taifa na kujiharibia soko wao wenyewe bila kujua," alisema
Mlundwa.
Nyota huyo wa zamani wa kimataifa wa ngumi, alisema siyo
kweli kama kuna rushwa zinazofanyika bali Watanzania wanaopewa nafasi
kulingana na rekodi zao nchini huenda kupigana kichovu kwa kukosa
maandalizi mazuri.
Ustaadh yeye alisema
 |
Francis Cheka |
linalowaangusha mabondia wa Tanzania nje ya nchi ni maisha wanayoishi
kuwa kinyume na nidhamu ya ngumi za kulipwa na kwamba kutokuwa na
mameneja ni tatizo jingine linalowakwaza.
"Mabondia wengi hawafanyi
mazoezi mpaka wakati wa pambano, hapo unatarajia afanye vizuri? Pia
hawaishi kwa kuzingatia miiko ya ngumi na hivyo wanapoenda nje ni rahisi
kupigwa na kuhisiwa labda wanauza," anasema.
Alisema ni vyema mabondia wakafanya kazi chini ya mameneja kama
ilivyokuwa kwa Rashid Matumla kwani itafanya ajikite kwenye mazoezi tu
na mambo mengine kuwaachia meneja zao.
Ustaadh alisema majukumu
wanayobeba mabondia ya kufanya kila kitu wakati mwingine huwafanya
washindwe kujikita kwenye mazoezi na hivyo kujikuta muda wa pambano
ukifika hawajajiandaa vizuri.
Rais huyo wa TPBO-Limited, alisema pia
mabondia wengi hutoa visingizio kila wanapopigwa nje ya nchi bila
kuangalia kama sheria za ngumi zinasemaje wanapokuwa kwenye ulingo na
kutolea mfano pigano la Cheka na Arik.
"Cheka alipolalamika
nilimuuliza vipi katika pambano lake na Arik, hakutupa ngumi yoyote
katika raundi ya 7 na kupigwa makonde mfululizo na kunieleza mkono wa
kulia ulimzingua, sheria zinasema bondia asipojibu mapigo kwa zaidi ya
ngumi 10 alizorushiwa refa anaweza kuvunja pambano au wasaidizi wa
bondia kuingilia kati kwa kurusha kitaulo na ndivyo ilivyotokea,"
alisema.
 |
Mada Maugo |