Tangazo

Pages

Wednesday, December 16, 2015

VICENT MBILINYI Bondia anayejipanga 'kumpopoa' Deo Njiku Desemba 25

Kocha wa kimataifa wa mchezo wa masumbwi nchini Rajabu Mhamila 'Super D' kushoto akimnowa bondia Vicent Mbilinyi wakati wa mazoezi yake ya kujiandaa na mpambano wake wa desemba 25 na deo Njiku utakaofanyika jamuhuri mkoa wa Morogoro Picha na SUPER D BOXING NEWS
VICENT MBILINYI
Bondia anayejipanga 'kumpopoa' Deo Njiku Desemba 25
NA MWANDISHI WETU

UWANJA wa Jamhuri mjini Morogoro, utakuwa mwenyeji wa mapambano kadhaa ya masumbwi, yatakayofanyika Desemba 25 mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za Sikukuu ya Krimas.
Moja ya mapambano yatakayorindima siku hiyo ni pamoja na lile linalomuhusisha Vicent Mbilinyi, atakayetoana jasho na Deo Njiku, pambano lisilo la ubingwa la uzito wa kilo 53, linalovuta hisia za wengi miongoni mwa mashabiki wa masumbwi.
Mvuto wa pambano hilo unatokana na ukweli kuwa, linakutanisha mabondia wa vizazi tofauti, Mbilinyi akiwa ni bondia wa kizazi cha sasa, wakati Njiku akiwa mmoja wa mabondia wakongwe.
Tanzania Daima limefanya mahojiano mafupi na Mbilinyi kuataka kujua alivyojipanga kuelekea pambano hilo, ambapo alisema maandalizi yake ni ya hali ya juu, nia ikiwa ni kuhitimisha utawala wa mabondia wakongwe.
"Niko kwenye mazoezi makali, chini ya kocha wangu Rajabu Mhamila 'Super D'. Nia ni kushinda pambano hilo na kutanua rekodi yangu ya mapambano niliyoshinda.
"Lakini pia, nataka kuhakikisha namchapa Njiku, ili sio tu kujenga heshima yangu, bali pia kumaliza utawala wa mabondia wakonge nchini. Hii itaongeza molari miongoni mwa mabondia vijana nchini," anasisitiza Mbilinyi

MSUKUMO KATIKA MASUMBWI

Katika miaka ya hivi karibuni takwimu zinaonesha kuwa masumbwi ndio mchezo wenye kuingiza pesa nyingi kuliko mchezo wowote duniani, ambapo kwa hivi sasa kinara wa utajiri kupitia mchezo huo ni bondia Floyd Mayweather.
Mkali huyo anafuatiwa na Manny Paquaio ambao wote ni mabondia wanaoshikilia nafasi mbili za juu za utajiri michezoni, huku  michezo mingine ikifuata.
Hiyo ndio sababu ya vijana wengi kuhamasika kujitosa katika mchezo huo, mmoja wapo akiwa kijana wa Kitanzania Vicent Mbilinyi, aliyezaliwa Septemba 5, 1992 mjini Musoma mkoani Mara akiwa ni mtoto wa nne katika ya sita wa mzee Alphonce Mbilinyi.
Alipata elimu yake ya msingi kuanzia mwaka 1999 katika Shule ya Mzimuni iliyopo Magomeni Dar es Salaam na kumaliza mwaka 2015.
Bondia huyu mahiri kwa ssa, hakupata bahati ya kuendelea na masomo kutokana na ukata wa familia, ambao ulimlazimu kuishia hapo, akiwa tayari ana damu za ubondia kutokana na kuupenda mchezo tangu akiwa anasoma darasa la kwanza.
Katika mahojiano na gazeti hili, Mbilinyi alisema alianza kupenda mchezo huo akivutiwa sana na kocha Sako Mwaisege 'Dungu' ambaye alikuwa akifanya mazoezi ya ngumi na kujiunga naye kama kocha wake wa mtaani pale maeneo ya Magomeni.
Baada ya kujifua sana kwa mazoezi na mbinu mbalimbali, kocha huyo alimpeleka katika timu ya Ngome pale Mwenge alipokutana na kocha Thimos Kingu na baada ya kupigana sana katika mashindano ya ridhaa na kukomaa katika mchezo wa masumbwi
"Baadae mazoezi ya Ngome yakanishinda, ambapo nilikuwa naishi Kibaha, Pwani kwa hiyo nilikuwa natumia shilingi 5,000 nikawa nimeshindwa kutokana kukosa mtu wa kuniwezesha katika swala la nauli," anasema.
Mbilinyi anaeleza kuwa baada ya kutoka Ngome, kocha Sako Mwaisege akampeleka moja kwa moja kwa kocha wa kimataifa wa mchezo wa masumbwi nchini, Super D ambaye mpaka sasa anampa makali ya mchezo huo.
Jukumu kuu la Super D likiwa sio tu kumfundisha, bali pia kumtafutia mapambano mbalimbali ndani na nje ya nchi, ingawa hajaanza kutoka nje ya mipaka ya Tanzania, ila anategemea ipo siku atakuja kuvuka kwa ajili ya mchezo wa masumbwi.
Pambano la kwanza la Mbilinyi, katika ngumi za kulipwa lilipigwa Januari 30 katika Ukumbi wa Manyara Park, ambako alipambana na Kulwa Bushiri.
Mpaka na sasa Mbilinyi amecheza mapambano nane, akishinda matano kati ya hayo, ametoka sare mapambano mawili na kupigwa pambano moja, rekodi inayompa matumaini ya kuzidi kufanya makubwa.
Baadhi ya mabondia aliocheza nao ni Kelvin Majiba, Khalid Hongo, Saidi Mundi, Yusufu Mkali, Epison John, Haridi Manjee.

WITO KWA WADAU WA MASUMBWI

Bondia huyo anayaomba makampuni mbalimbali kujitokeza kufadhili mchezo wa ngumi kama wanavyofanya katika michezo mingine, ambayo mpaka sasa ina wafadhili wengi hivyo kuwataka wengine wageukie masumbwi.
Anabainisha kuwa, iwapo wafadhili watajitokeza kwa wingi, kutasaidia vijana wengi kufikia malengo sio tu ya kuliletea sifa taifa, bali pia kujikwamua kiuchumi, hasa ukizingatia kwa sasa michezo, hususani ubondia ni ajira wanayoitegemea.
Bondia huyo pia ametoa wito kwa vijana mbalimbali kujiunga na mchezo wa ngumi, kwani kwa sasa unalipa, kama inavyothibitishwa sio tu na kina Mayweather na Pacquiao, bali pia vijana kibao wa Kitanzania ambao wameanza kufanikiwa kupitia ngumi.
Mbilinyi anaenda mbali zaidi kwa kuwashauri vijana kuacha uasherati na matumizi ya dawa za kulevya na uvutaji wa bangi, kwani unapunguza nguvu na kurudisha nyuma harakati za kimaendeleo za vijana, hasa wanamichezo.

WASIFU:
JINA KAMLI: Vicenti Mbilinyi
KUZALIWA: Septemba 5, 1992
ALIKOZALIWA: Musoma, Mara
MCHEZO: Ngumi za Kulipwa
MAPAMBANO: Nane


Kocha wa kimataifa wa mchezo wa masumbwi nchini Rajabu Mhamila 'Super D' kulia akimnoa bondia Vicent Mbilinyi wakati wa mazoezi ya kujiandaa kupambana na Deo Njiku mpambano utakaofanyika siku ya desemba 25 katika uwanja wa jamuhuri Morogoro Picha na SUPER D BOXING NEWS



Kocha wa kimataifa wa mchezio wa masumbwi nchini Rajabu Mhamila 'Super D' akifanya mazoezi ya nguvu na bondia Vicent Mbilinyi anaejiandaa kutwangana na Deo Njiku siku ya Desemba 25 katika uwanja wa jamuhuri Morogoro Picha na SUPER D BOXING NEWS

No comments:

Post a Comment