(ULINGO)
Buster amduwaza Mike Tyson
FEBRUARI 11 mwaka 1990 jijini Tokyo nchini Japan, Mike Tyson alipoteza pambano lake la kwanza kwa Buster Douglas, ingawa alikuwa anapewa nafasi kubwa ya kushinda.
Lakini kikubwa ambacho wengi hawakijui ni kwamba, Douglas alipanda ulingoni katika pambano hilo ikiwa ni siku 23 tu baada ya kumpoteza mama yake mzazi.
Mama yake Douglas, Lula Pearl alifariki siku 23 kabla ya pambano hilo baada ya kupatwa na ugonjwa wa kiharusi.
Hali hiyo mashabiki wengi waliichukulia kwamba ingempotezea kujiamini Douglas katika pambano na hivyo walikuwa na imani kubwa ya kulipoteza.
Wakati pambano hili linaanza, kambi ya Tyson ilikuwa ikishangilia kwa nguvu huku ikiamini kwamba atashinda kwa urahisi, hasa ikizingatiwa kwamba alikuwa hajawahi kupigwa tangu aanze masumbwi ya kulipwa ya uzito wa juu.
Tyson alifanikiwa kumpeleka chini Douglas katika raundi ya nane na hapo ndipo wengi waliamini mwisho wake umefika, lakini alihesabiwa na kufanikiwa kusimama.
Douglas alinyanyuka akiwa na nguvu ya ajabu, kwani katika raundi ya 10 alifanikiwa kusukumizia makonde mazito Tyson na kumpeleka chini ya sakafu.
Kudondoka kwa Tyson katika raundi hiyo, ndiyo ilikuwa ni mara yake ya kwanza katika kipindi chake cha uchezaji wa ndondi.
Mwamuzi wa pambano hilo Octavio Meyran alimhesabia mara 10 Tyson, lakini alishindwa kusimama na hivyo Douglas akatangazwa bingwa mpya.
Hata hivyo, kambi ya Tyson ilimlalamikia mwamuzi huyo kwamba alimhesabia kwa haraka, wakati kwa Douglas hakufanya hivyo wakati amedondoka.
Wengi waliamini kwamba Tyson aliathirika kisaikolojia kwa kushindwa kuamini kama amedondoshwa na hivyo kujikuta akiwa hana uwezo wa kusimama haraka.
Kipigo hicho cha Tyson ndiyo kinachukuliwa kuwa cha kushitukiza zaidi katika historia ya mchezo wa masumbwi duniani.
Aidha kipigo hicho cha Tyson kilikuja wakati ambao akishikilia mikanda mikubwa mitatu ya uzito wa juu duniani ambayo ni WBC, WBA na IBF.
Lakini kubwa zaidi ni kwamba Tyson alikuwa akipanda ulingoni katika pambano hilo akiwa na mahusiano mabaya na Robin Givens kiasi kilichochangia kutokuwa na maelewao mazuri na Meneja wake wa muda mrefu, Bill Cayton pamoja na promota wake Don King.
Pia Tyson alikuwa anatoka kumtema mkufunzi wake wa mazoezi wa muda mrefu, Kevin Rooney.
Tyson alipanda ulingoni kwenye pambano hilo akitoka kumchapa Carl William kwa KO kwa sekunde 93.
Na pambano hilo la Douglas lilichukuliwa kama ni la kujipima nguvu kabla ya kumvaa Evander Holyfield ambaye alijipambanua kutaka kupanda naye ulingoni.
No comments:
Post a Comment