Tangazo

Pages

Thursday, September 15, 2016

JIFUNZE MASUMBWI NA SUPER D COACH

ULINGO
 
Pambano la Alfa na  Sorkitti ilikuwa balaa
 
HILI lilikuwa ni pambano kali kati ya  Muhammad Alfaridzi akijulikana maarufu kwa jina la ‘ Alfa’ lilikuwa dhidi ya Kongthawat Sorkitti aliyejulikana kwa jina la Thongchai Treeviset.
 
 Lilikuwa ni pambano kali lililofanyika Machi 30, 2004 ambapo Muhammad Alfaridzi, alisimamishwa katika raundi ya 8 kwa  KO. Kumbuka Alfaridzi aliyezaliwa Agosti 2, 1976 alikuwa anatimiza mika 25 wakati mpinzani wake wakati huo alikuwa na miaka 30.
 
Pambano
 
Lilikuwa ni pambano kali na la mchakamchaka, lakini ‘siku ya mwisho’ Kongthawat Sorkitti akaibuka na ushindi baada ya kumsimamisha Alfaridzi kwa ‘Knockout’ (KO) ya raundi ya nane na kutwaa ubingwa wa super featherweight.
 
 Raundi ya kwanza:
 
Kongthawat Sorkitti anaanza taratibu raundi huku Alfaridzi akionekana kukamia zaidi na kusukuma masumbwi kutaka kumaliza pambano mapema. ‘Jab’ za Alfaridzi zinatembea na zinamkamata Sorkitti, kwa muda mwingi Alfaridzi anatawala pambano na raundi ya kwanza inamalizika Alfaridzi akiongoza kwa pointi.
 
 Raundi ya pili na tatu:
 
Raundi ya pili  na tatu haikuwa tofauti na ya kwanza, katika raundi hizi mbili, Alfaridzi anaendelea kumshambulia Sorkitti kwa kutumia ‘jabs’ na ngumi mchanganyiko na Sorkitt anatumia muda mwingi kujihami na kurusha ngumi moja moja lakini kwa umakini mkubwa, raundi ya tatu kama zilivyo za pili na kwanza zinamalizika na Alfaridzi anakwenda kwenye kona akiwa na anaongoza kwa pointi.
 
 Raundi ya nne:
 
Raundi ya nne inabadilika, Sorkitti anaibuka na kuanza kusukuma makonde mazito, Alfaridzi anajaribu kumpunguza kasi lakini inakuwa si rahisi,  uzoefu unaonekana kumbeba zaidi Sorkitti, anatupa makonde ya uhakika zaidi na yanamkamata vizuri Alfaridzi na raundi inapomalizika Sorkitti anaongoza kwa pointi.
 
  Raundi ya tano na sita
  Raundi ya tano, Sorkitti anaendelea kusukuma makonde mazito kwa  Alfaridzi. Alfaridzi anapiga jab zake na ngumi zake za kulia ‘right’, lakini Sorkitti hampi nafasi, anambana Alfaridzi na kumpa kibano cha uhakika.
 
Raundi ya sita, kama ilivyokuwa raundi ya tano, Sorkitti anasukuma makonde mazito kwa Alfaridzi anayejikinga asiendelee kunyeshewa mvua za ngumi, Sorkitti anaonekana kupata nguvu zaidi na kuzidi kumpelekesha  Alfaridzi na sasa akipigana kwa nia ya ushindi zaidi, anapiga ngumi nzito na zinatua kichwani kwa Alfaridzi, raundi inamalizika Sorkiti anaongoza kwa pointi.
 
  Raundi ya saba:
 
Katika raundi hii, Alfaridzi anazidiwa dhahiri, anapokea makonde ambayo yanamzidi ‘umri’, Sorkitti anapiga ngumi ya kushoto inamkamata Alfaridzi, anapiga ya kulia inamkamata pia Alfaridzi, anayeyumba huku na kule na kusimama lakini kwa ‘mawenge’ akiendelea kukomaa lakini Sorkitti anasukuma ‘jab- jab’  kisha ‘right’ na kengele inalia kumaliza raundi hiyo na Sorkitti akiongoza tena raundi hiyo.
 
Raundi ya nane:
 
Sorkitti anaanza kwa nguvu zaidi na kumsukumia makonde Alfaridzi akitumia jab na ngumi mchanganyiko ‘combination’, anapiga ngumi ya kushoto ‘left’ kisha anaachia ngumi mkunjo kali ya kulia ‘rigt hok’ na inatua kwenye taya la Alfaridzi na anakwenda chini kama gunia la nyanya.
 
 Mwamuzi anamuhesabia, lakini inapofika sita, Alfaridzi haoneshi dalili za kusimama, timu yake kwenye kona inakimbilia ulingoni na kwa haraka wanamvua viatu na glavu na kuanza kumpepea wakimpa huduma ya kwanza bila mafanikio kwani Alfaridzi amepoteza fahamu kutokana na kipigo kile.
 
 Haraka Alfaridzi anakimbizwa hospitali ambako anafanyiwa upasuaji wa kichwa  na kuondolewa damu  iliyovia kwenye ubongo, lakini anabaki akiwa hana fahamu na akipumulia mashine kwa muda wa siku tatu na kisha kufariki dunia Aprili 2, 2004 akiwa na miaka 25.
 
 Kuna tetesi hata sasa kwamba bondia  Alfaridzi kabla ya pambano hilo alifanya fujo mtaani na watoto wa kihuni wakamtwanga fimbo kichwani. Siku chache baadaye akapanda ulingoni, hivyo kifo chake inasadikika kilianza na kupigwa kwake fimbo kichwani kwani huenda kulisababisha ufa kwenye fuvu la kichwa ambao uliongezewa na ngumi za Khongtawat Sorkitti siku ya pambano, kwani Alfaridzi hakuwahi kupima kichwa baada ya kupigwa fimbo ile mtaani.
 **Mwandishi ni kocha wa mchezo wa ngumi anayefundisha klabu mbalimbali Dar es Salaam. Anapatikana kwa simu 0713/0787- 406938 au email: superdboxingcoach@gmail.com

No comments:

Post a Comment