

Pacquiao
NA MITANDAO
WANAMICHEZO wawili maarufu duniani, bondia Manny Pacquiao na mcheza
tenisi, Maria Sharapova, wamejikuta wakipoteza mamilioni ya fedha
walizokuwa wakiingiza kupitia udhamini wao baada ya kuingia matatani na
wadhamini wao kwa mambo mawili tofauti.
Wakati Pacquiao ambaye ni mwanasiasa maarufu nchini kwao Ufilipino
akijikuta matatani kutokana na kauli yake aliyoitoa hivi karibuni kwa
kuwashambulia mashoha, Maria mapema wiki hii alilitia doa jina lake
kutokana na kashfa ya kutumia dawa zilizokatazwa michezoni.
Katika maoni yake hayo dhidi ya mashoga aliyoyatoa wakati wa mahojiano
na kituo cha televisheni cha Ufilipino, ambako anawania nafasi ya
useneta kuelekea uchaguzi wa Mei mwaka huu, Pacquiao mwenye umri wa
miaka 37, alisema: “Ni hali ya kawaida. Huwa unaona wanyama wa jinsia
moja wakifanya ngono?
“Wanyama ni bora zaidi kwasababu wanaweza kutofautisha mwanamke na
mwanaume. Iwapo mwanaume anafanya ngono na mwanaume mwenzake na mwanamke
anashiriki tendo hilo la ngono na mwanamke mwenzake, ni wabaya zaidi ya
wanyamya.”
Na akiwa anajiandaa kupanda ulingoni kwa mara ya mwisho dhidi ya Timothy
Bradley Aprili 9, mwaka huu, bondia huyo amejikuta akipata pigo baada
ya wadhamini wake, kampuni ya Nike kuvunja mkataba baina ya pande hizo
mbili.
Nike walitoa taarifa yao huu ya uamuzi wao huo, iliyosomeka: “Tumebaini
maoni ya Manny Pacquiao yamepingana na mawazo ya wengine.
“Nike tungapinga kwa nguvu zote ubaguzi wa aina yoyote na imekuwa na
historia ndefu ya kusapoti kusimamia haki za jamii ya watu wenye
uhusiano wa jinsia moja. Kuanzia sasa hatuna uhusiano wowote na Manny
Pacquiao.”
Hata hivyo, Pacquiao aliomba msamaha uliotajwa kuwa dhaifu, akisema:
“Samahani kwa kuwaumiza watu kwa kulinganisha mapenzi ya jinsi moja na
wanyama. Niliowaumizi naomba wanisamehe tafadhali.
“Bado ninasimama katika imani yangu kuwa ninapingana na ndoa za jinsia
moja kwasababu ya kile Biblia inachosema. Ninawapenda wote kwa mapenzi
ya Mungu. Mungu awabariki wote na ninawaombea.”
Na anapojiandaa kushuka dimbani kwa mara ya mwisho, ni wazi kuwa kujitoa
kwa wadhamini wake kutokana na maoni yake hayo dhidi ya mashoga,
kutakuwa kumemwathiri kwa kiasi kikubwa katika suala zima la kimaslahi,
lakini pia harakati zake za kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Ufilipino.
Kwa upande wake, Maria Sharapova amejikuta kwenye hasara kubwa ya
maisha yake baada ya kupoteza dili lake na Nike lenye thamani ya Dola za
Marekani milioni 70 ndani ya saa moja tu baada ya kutangaza kuwa
amekutwa ametumia dawa ambazo hazitakiwi kwa wanamichezo.
Maria amebainika kutumia dawa ambazo haziruhusiwi kwenye michezo ambazo
amezitaja kama mildronate au meldonium kuanzia Januari mwaka huu baada
ya kufanyiwa vipimo.
Baada ya habari hizo kutoka, wadhamini wake wakaanza kuvunja mikataba,
kuanzia Nike ambao ndio walikua na dili kubwa la Dola hizo za Marekani
milioni 70, kabla ya kampuni ya nembo za saa za mkononi za TAG Heuer nao
kujitoa kumdhamini mwanadada huyo wa Urusi.
Msemaji wa Nike amesema: “Tumesitisha kufanya kazi na Sharapova kwa wakati huu tukiendelea na uchunguzi hadi hapo baadaye.”
Kutokana na takwimu za Forbes, Sharapova alikua akipokea Dola za
Marekani milioni 30 kwa mwaka kutokana na mishahara mbalimbali na kwamba
fedha hizo zinatarajiwa kushuka kutokana na wadhamini wake kuvunja
mikataba.
Kwa upande mwingine, kitendo cha Nike kusitisha mikataba na wanamichezo
hao, kimepokewa kwa hisia tofauti duniani kote, ikiwamo hapa Tanzania,
baadhi wakiwasapoti, huku wengine wakiwashangaa kwa uamuzi wao huo
wakidai umelenga katika kukomoana.
Mmoja wa wadau maarufu wa ndondi nchini Tanzania, Rajab Mhamila ‘Super
D’, alisema: “Watu wengi wana hobi zao, Manny Pacquiao hajatoa maoni
yake kwa kubuni tu, ametoa mistari katika Biblia kuwa hakuna mapenzi ya
jinsia moja, kasimamia katika ukweli na uhakika, huwezi kupinga ukweli,
inawezekana kuna watu ndani ya Nike hawajafurahishwa na maoni yake.
“Pacquiao ni mtu wa Mungu ndio maana hata katika mapambano yake lazima
utamuona akiwa amevaa msalaba, anasimamia imani yake na ndio maana
alitoa vifungu vya mistari katika utetezi wake akisema sisi binadamu
tumekuwa wabaya zaidi ya wanyama ambao hawawezi kufanya vitendo hivyo
wanavyofanya baadhi ya binadamu. Mimi nipo upande wa Pacquiao.”
Hata katika mitandao mbalimbali ya kijamii ya Tweeter, Instagram,
facebook na mingineyo, wapo wachache mno waliosapoti uamuzi wa Nike
dhidi ya Pacquiao na Maria, huku wengi wakionekana kuiponda kampuni hiyo
kwa kukurupuka katika maamuzi yao, hasa kitendo cha kumtosa Pacquiao.