Tangazo

Pages

Wednesday, April 6, 2016

EUBANK Familia ya magwiji wa ndondi *Wapiga wapinzani mpaka kuzimia *Baba alipiga 1991, mwanawe juzi

Bondia Chris Eubank JR akimwangalia mpinzani wake
Nick Blackwell baada ya kumpeleka chini kwa makonde mazito
Bondia Chris Eubank JR kushoto akipambana na Nick Blackwell  

 baba na mwana
 Bondia Chris Eubank JR


Bondia Chris Eubank SR akimwelekezaBondia Chris Eubank JR jinsi ya kupiga ngumi zito na zenye shabaha

EUBANK
Familia ya magwiji wa ndondi

 *Wapiga wapinzani mpaka kuzimia
*Baba alipiga 1991, mwanawe juzi

LONDON, Uingereza

NI karibu miaka 25 sasa tangu mwanamasumbwi, Chris Eubank alivyomwacha mpinzani wake akiwa mahututi, baada ya pambano lao lililosababisha maoni ya kutaka mchezo huo upigwe marufuku.

Mwishoni mwa wiki alionekana shujaa baada ya kuingilia kati tukio kama hilo ambapo mwanawe Chris Eubank Jr, alimjeruhi vibaya mpinzani wake  hata kumfanya apoteze fahamu ulingoni.

Nick Blackwell (25), ambaye alivuja damu kwenye ubongo, alilazimika kuondolewa kwenye ulingo katika Uwanja wa Wembley Arena akiwa kwenye machela na kukimbizwa hospitalini ambako aliendelea kufanyiwa uchunguzi.

Eubank Sr alikuwa pembeni mwa ulingo Jumamosi na alithubutu kuokoa maisha ya Blackwell kwa kumtaka mwanawe kumpiga mwilini badala ya usoni, katika raundi mbili za mwisho na kusema kuwa  mwamuzi alitakiwa kumaliza pambano hilo.

Alifikia hatua ya kupiga sakafu ya ulingo katika jaribio la kumtaka mwamuzi Victor Loughlin amalize pambano lile.

Katika raundi ya nane, Eubank Sr alimweleza mwanawe asimlenge Blackwell kichwani na badala yake ampige mwilini tu.

Pambano hilo hatimaye lilisimamishwa katika raundi ya 10 baada ya daktari kumshauri mwamuzi kwamba mtetezi wa pambano lile Blackwell hakuwa na uwezo wa kuona kwa jicho lake la kushoto na Eubank Jr (26) akatwaa ubingwa wa Uingereza.

Huku kukiwa na vilio vya wasiwasi wa kuhatarisha maisha ya wanamasumbwi, kulikuwa na sifa pia kwa Eubank Sr (49). Ujumbe kutoka kwa mtumiaji wa mtandao wa Twitter ulisema: "Chris Eubank Sr angeweza kuokoa maisha ya Blackwell usiku wa jana."

Kazi hiyo ya mwisho ya mwanamasumbwi huyo aliyestaafu, ilirejea katika kumbukumbu za usiku wa Tottenham, London Kaskazini mwaka 1991 alipomfanya Michael Watson kuzimia kwa siku 40. Watson ambaye alipata madhara kwenye ubongo, alizinduka lakini amekuwa mlemavu tangu hapo.

Jumamosi usiku Eubank Jr alikuwa akiongoza hadi raundi ya nane pale baba yake alipoingia ulingoni na kumpa ushauri.

Kamera za runinga zilimnasa akimwambia mwanawe huyo: "Kama mwamuzi hatasimamisha pambano, sijui cha kukwambia, lakini nakwambia hivi: Moja, kama hatasimamisha pambano na tukaendelea kumpiga kama hivi, ataumia; mbili, kama hataamua, sioni kwa nini asisimamishe pambano? Sielewi ni kwa nini?

"Pengine hili usimwachie mwamuzi. Ni vema usimpige zaidi usoni - mpige mwilini tu."

Makonde ya Eubank yalipungua katika raundi mbili za mwisho na mashabiki wengi wa ndondi kupitia Twitter walisema ushauri wa Eubank Sr kwa mwanawe uliokoa maisha ya Blackwell.

Mara baada ya pambano kusimamishwa, Blackwell, kutoka Wiltshire, ambaye alikuwa akivuja damu puani, ghafla alianguka ulingoni. Mara moja alianza kupewa huduma za kitabibu.

Mashabiki hao kupitia Twitter walisema mwamuzi au makocha wa Blackwell walipaswa kusimamisha pambano mapema.
 
Gwiji wa michezo Pilib de Brun aliandika kwenye Twitter: "Haiaminiki ni kwa jinsi gani pambano lile halikusimamishwa mapema! Blackwell ni kijana mgumu kwelikweli."

Wapenzi wa Best of Boxing katika ukurasa wao walisema: "Sote tunajua hatari iliyomo katika masumbwi hata hivyo mwamuzi au makocha wa Blackwell wangekuwa wamesimamisha pambano mapema."

Kikundi kinachojihusisha na majeraha ya ubongo kinachojiita Headsmatter kiliandika: "Hali ya Nick Blackwell inaongeza uzito katika hatari walizonazo wanamasumbwi ... hii ilitakiwa kusimamishwa mapema."

Eubank Sr alimshauri mwanawe kuacha kumpiga Backwell kichwani, akikumbuka uzoefu wake baada ya kumwacha Watson amezimia miaka 25 iliyopita.

Katibu Mkuu wa Bodi ya Udhibiti wa Ndondi Uingereza, Robert Smith akimzungumzia Blackwell Jumapili, alisema: "Yuko katika uangalizi maalumu, amewekewa nusu kaputi na anapumzika na kufuatiliwa.

"Ni utaratibu wa kawaida. Wanakuwekea nusu kaputi ili uvimbe upungue. hatuwezi kusema muda gani atazinduka. Ni suala la kusubiri na kuona."

Baadaye Smith alimtetea mwamuzi Loughlin, ambaye alisema alifanya 'kazi nzuri.'

Smith aliambia BBC: "Nimezungumza na mwamuzi, Loughlin, nimezungumza na Gary Lockett (Kocha wa Blackwell). Tulikuwa na mjadala kuhusu ni jinsi gani mpambano huo ulikwenda na nimeridhishwa na uamuzi wao wa usiku huo.

Aliongeza: "Kila mwanamasumbwi anayeingia ulingoni anazijua hatari zake. Huwa tuna maandalizi mazuri tu kiasi tunachoweza, lakini hatuwezi kuondoa hatari zote...hatuwezi kuwa na uhakika wa usalama kwa asilimia 100.

"Tuna wataalamu wa kila aina pale, tuna wauguzi, tuna madaktari. Tunawasiliana na vituo vya karibu vya wataalamu wa fahamu. Tunafanya kila kitu kinachowezekana. Tuko makini sana katika nchi hii.

"Ndivyo ulivyo mchezo wenyewe. Tunaishi nao hivyo na tunauelewa.  Nick Blackwell alitaka kuwa mwanamasumbwi, kama mtu yeyote anayetaka kushiriki ndondi. Sote tunajua hatari zake."

Alisema Eubank Sr alitilia shaka uamuzi wake, lakini akasema kulikuwa na watu wengi wenye uzoefu pale ambao waliona mwamuzi alichukua uamuzi mzuri.

Eubank Jr, kutoka Brighton, alisema baada ya pambano lake: "Nilimpiga ngumi nzito , yawezekana mwamuzi angesimamisha pambano mapema.  Naheshimu mtu yeyote anayepanda ulingoni. Inasikitisha kuwa aliondoka kwa machela."

Watson, ambaye alianguka na kupoteza fahamu katika pambano lake na Eubank Sr mwaka 1991 alizimia kwa siku 40 na kufanyiwa upasuaji mara sita ili kuondoa damu iliyoganda kwenye ubongo wake.

Aliandika kwenye gazeti la Telegraph: "Nilipoteza kumbukumbu kabisa. Lilikuwa jambo jipya kumwona Chris kwenye kona na mwanawe, na nimeshashuhudia mapambano mengi ya Chris. 
"Chris na Nick walipambana vikali na lilikuwa jambo la kuhuzunisha kumwona Nick amajeruhiwa mwishowe na kisha kusikia kilichomsibu baada ya pambano. Hakika lilikuwa jambo la kushtua kusikia kilichoendelea.

"Ni wazi namtakia Nick na familia yake mapenzi na maombi wakati huu mgumu ambao anahudumiwa hospitalini."

Blackwell alipambana kiume lakini hakuweza kumudu nguvu na adhabu aliyopata kutoka kwa Eubank.

Eubank alionekana kuchoka katika hatua za mwisho lakini alibadilika na kuweza kupata ushindi kirahisi.

No comments:

Post a Comment